Kesi ya Malkia wa meno ya tembo kusikilizwa Tanga

Muktasari:

Watuhumiwa watatu wanadaiwa kupanga na kutekeleza biashara hiyo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Mei 17, 2018  imeridhia maombi ya upande wa Jamhuri kwenda kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi  inayowakabili washtakiwa watatu akiwamo Malkia wa meno ya tembo, Muheza Mkoa wa Tanga.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwa baadhi ya vielelezo katika kesi hiyo vipo mkoani Tanga.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Salvius Matembo, Philemon Manase na raia wa China  Yang Feng Glan (66), anayedaiwa kuwa ni Malkia wa meno ya tembo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh13 bilioni, kinyume cha sheria.

Hakimu Shahidi amesema Mahakama hiyo itafanya utaratibu unaotakiwa kwa ajili ya kupata kibali cha kuhamisha kesi hiyo kwa muda kutoka Dar es Salaam hadi Muhenza kwa ajili ya usikilizwaji.