Kesi ya Mwanyika yapigwa kalenda

Friday November 22 2019

By Pamela Chilongola, Mwananchi pchilongol[email protected]

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili, Deo Mwanyika imeahirishwa baada ya hakimu anayeisikiliza kuwa nje ya Jiji la Dar es Salaam kikazi.

Mwanyika alikuwa Rais wa migodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Leo Ijumaa Novemba 22, 2019 wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini  hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina yupo nje ya Mkoa kikazi.

“Upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika, tunaiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Simon.

Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6, 2019.

Mbali na Mwanyika, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja uhusiano wa mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo; mkurugenzi mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku, Assa Mwaipopo; kampuni ya mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Advertisement

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya Dola 112 milioni za Marekani.

Pia wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, saba ya kughushi, 17 ya utakatishaji wa fedha, kuwasilisha nyaraka za uongo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), shtaka moja la kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka manane ya kukwepa kodi na moja la kutoa rushwa.

Advertisement