Kesi za ufisadi kutumia miezi 9

Muktasari:

Awali, wadau wa mapambano dhidi ya rushwa walikuwa na hofu kuwa kesi hizo zingeweza kuchukua muda mrefu kumalizika. Mbali ya wadau hao, vyama vya siasa vimekuwa vikielezea kuhusu hofu hiyo. Wiki iliyopita, Chama cha Wananchi (CUF) kilimpongeza Rais John Magufuli kuanzisha Mahakama hiyo, huku kikitaka itakapoanza isiwe na upendeleo wala kutumika kuwamaliza wanasiasa wanaoonekana kuwa tishio kwa uchaguzi wa 2020.

Dar es Salaam. Takriban siku 88 zikiwa zimepita tangu Bunge lipitishe muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwamo kuanzisha Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imefahamika sasa kesi za watuhumiwa ufisadi hazitachukua zaidi ya miezi tisa katika Mahakama hiyo.

Awali, wadau wa mapambano dhidi ya rushwa walikuwa na hofu kuwa kesi hizo zingeweza kuchukua muda mrefu kumalizika. Mbali ya wadau hao, vyama vya siasa vimekuwa vikielezea kuhusu hofu hiyo. Wiki iliyopita, Chama cha Wananchi (CUF) kilimpongeza Rais John Magufuli kuanzisha Mahakama hiyo, huku kikitaka itakapoanza isiwe na upendeleo wala kutumika kuwamaliza wanasiasa wanaoonekana kuwa tishio kwa uchaguzi wa 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, jana, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande aliweka wazi kanuni za mahakama hiyo zitakazotumika, huku akisema katika mazingira ya kawaida kesi hizo hazitachukua zaidi ya miezi tisa tangu kufunguliwa hadi kutolewa hukumu.

Jaji Chande alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania pamoja na mradi wa maboresho ya huduma za Mahakama.

Akizungumzia kanuni hizo zinazojulikana kama The Economic and Organise Crime Control (Corruption and Economic Crime Division) Procedure Rules of 2016, Jaji Chande alisema tayari zimekamilika ikiwa ni pamoja na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali kupitia tangazo la Serikali (GN) la Septemba 9, 2016.

Alisema kwamba kanuni hizo zinaeleza namna ya kufungua kesi hizo na kwa jina gani, kuwalinda mashahidi na kwamba kesi inapofunguliwa ndani ya siku moja zinakwenda kwa majaji watakaozisikiliza.

Jaji Chande aliongeza kuwa usikilizwaji wa awali wa kesi hizo utafanyika ndani ya siku 30 na kwamba kesi hizo zitakuwa zinamalizika ndani ya miezi tisa.

“Kama kuna sababu zisizoepukika basi itaongezwa miezi sita,” alisema Jaji Chande na kuongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni hizo, kama kuna ucheleweshaji wa makusudi itajulikana anayechelewesha na hivyo kuweza kuwajibishana hata kama ni Mahakama au wakili.

Akizungumzia mpango huo utakaogharimu Sh238 bilioni ambao utazinduliwa kesho na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu alisema hiyo ni dira ya Mahakama nchini iliyojiwekea itakayoiongoza katika kutoa haki na kwa wakati.

Jaji Chande alisema mpango mkakati huo utahusisha mageuzi ya teknolojia katika kusikiliza kesi na mahakama inalenga kuhama kutoka mfumo wa kuweka kumbukumbu za mwenendo wa kesi kwa kuandika kwenye karatasi kutumia mashine.

Pia, alisema katika mageuzi hayo teknolojia inalenga kumwezesha mwananchi kufungua kesi kwa njia ya mtandao.la ya kulazimika kubeba makabrasha kwenda kwa msajili.