VIDEO: Hiki ndicho kilichowaponza, Kakunda, Kichere

Tuesday June 11 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza kuwa sababu za kumng’oa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda ni suala la korosho na kilichomponza Charles Kichere aliyekuwa TRA ni kushindwa kukusanya mapato pamoja na kufuata maelekezo.

Alisema Kakunda alishindwa kutafuta soko la korosho za msimu wa mwaka jana huku Kichere akishindwa kufuata nyayo za Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyekaimu nafasi hiyo mwaka 2016 ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Rais Magufuli alieleza sababu hizo jana Ikulu Dar es Salaam wakati akimwapisha Innocent Mashungwa kuchukua nafasi iliyoachwa na Kakunda, Kichere kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe huku akimwapisha Edwin Mhede kuwa bosi mpya wa TRA.

Kakunda aliteuliwa Novemba 12, 2018 akimrithi Charles Mwijage ambaye pamoja na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba waliondolewa kwenye nyadhifa zao kwa kushindwa kupata mwafaka wa biashara ya korosho.

Serikali iliamua kununua korosho zote za wakulima kwa bei ya Sh3,300 baada ya kushindwa kuelewana na wafanyabiashara waliodaiwa kutaka kununua kwa bei ya chini.

Huku akizungumza kwa hisia kali, Rais Magufuli alisema alitamani kuwasimamisha kazi watumishi wa wizara yote, “una waziri wa biashara ana vyombo vyote vya kufanya biashara, Tantrade (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara), nani wote wako huko, ilitakiwa ‘actually’ niifagie kutoka juu mpaka chini huku.

Advertisement

“Pamoja na wewe Mhede ulikuwa uende kwa sababu ulikuwa hukohuko. Nasema kweli na hiyo ndiyo dhamira yangu.”

Akifafanua sababu ya kumwengua Kakunda, Rais alisema, “tumefanya biashara ya korosho hapa, tani 200,000 na kitu, ni ngapi zimeuzwa? Lakini wizara inaitwa Wizara ya Viwanda na Biashara, ni biashara gani imefanya?” alihoji Rais “Wizara ya Kilimo imefanya wajibu wake, imenunua. Wanajeshi wametimiza wajibu wamesomba korosho zote wameweka kwenye magodauni. Wizara ya Biashara imefanya nini?

“Korosho zile zimekaa wakati huo Tanzania tulikuwa tumezalisha korosho, tumekaa mwezi wa tatu, mpaka wa nne ukaingia. Nchi nyingine za Benin, Nigeria, Cote D’ivoire nazo zikazalisha, bado hatujauza. Sasa unakuwa na wizara la nini, kuipeperusha bendera barabarani?”

Mbali na suala la korosho, Rais Magufuli alihoji sababu ya wizara hiyo kutofanya mikutano na wafanyabiashara ili kujua kero zao.

“Changamoto za wafanyabiashara. Kwani palikuwa na ubaya gani, naibu waziri, katibu mkuu waziri mwenyewe, si wangekuwa wameshapanga mikutano na wafanyabiashara? Nani aliwakataza?” alihoji.

“Ukiulizwa, Wizara ya Kilimo ilikusanya korosho zote, tani 223,000 ziko kwenye magodauni, kwa hiyo kilimo wametimiza wajibu wao. Hii viwanda na biashara wamegbangua tani 2,000 hizi zingine wanasubiri mpaka nani ateremke ndiyo awaambie kwamba mnatakiwa amuuze korosho?”

Alimtaka Waziri Bashungwa kufanya kazi na asicheke na mtu na asiogope kuchukiwa na watu.

“Viwanda ambavyo vipo tu vitafutiwe watu wavichukue. Vile viwanda vikafanye ,” alisema.

TRA na Kichere

Mbali na Kakunda, Rais Magufuli alieleza sababu ya kumwondoa Kichere katika nafasi ya Kamishna Mkuu wa TRA, akisema alishindwa kufuata nyayo za Dk Mpango.

“(Dk Mpango) ndiye aliyepandisha (makusanyo) kutoka Sh850 bilioni mpaka Sh1.3 trilioni. Nikaona huyu safi anajua mipango, nikampa uwaziri, nimem-promote kutoka pale TRA. Sasa ninyi mmekuwa mkienda pale mmesimamia hapohapo kana kwamba ni fomula ya Mungu,” alisema Rais.

Mbali na ukusanyaji wa mapato, Rais Magufuli alisema alikuwa akimpelekea Kichere meseji za malalamiko ya walipa kodi lakini hakuyafanyia kazi.

“Tatizo complaints (malalamiko) nyingi na hamchukui hatua. Kama kuna meseji nime ku fowadia wewe Kamishna uliyeondoka inawezekani zinazidi 20, 30 zingine namfowadia saa nane za usiku, zingine saa tisa zingine saa 10,” alisema.

Aliongeza, “jamaa huyu ni kama diplomat (mwanadiplomasia) anasema nimepokea mheshimiwa, ukifuatilia hakuna matokeo. Ndiyo ukweli, mimi huwa sisahau ndiyo dhambi niliyonayo.”

Aliongeza kuwa kosa lingine ni kushindwa kuwawajibisha viongozi wake wa chini waliokuwa wakikadiria kimakosa kodi kwa wafanyabiashara.

“Unaona kabisa kuna wafanyabisahara wanapakia mizigo wanaiandika kwamba ni in transit (inayopita) kwamba inakwenda nchi za jirani, wanafika Tunduma wanagongewa mihuri, wanarudi kuishusha humo, wakati barabara yote TRA ipo. Umeshindwa hata ku ‘intercept’ (kuingilia).”

Aliendelea, “Sasa ndiyo maana nikasema kwa kweli siwezi na walipokusema siku ile nakuuliza wala hujui, unaangalia mtu wa nyuma yako. Ndiyo tumekupeleka huko (Njombe) na huko ukifanya vibaya tunakutoa. Tusifiche ndugu zangu,” Rais Magufuli alimwambia Kichere.

Akifafanua zaidi kuhusu mchezo huo, Rais Magufuli aliutaja mpaka wa Tunduma akihoji kama msimamizi wake ameshasimamishwa kwa kugonga mihuri kwenye mizigo ambayo haipelekwi nje ya nchi.

“Kuna mipaka inayofanya kazi vizuri, Rusumo anafanya kazi vizuri, lakini Tunduma hafai, Sirari hafai, wengine utajaza mwenyewe.

“Wa Tunduma sifahamu kama mmeshamtoa, yule ndiyo aliyekuwa ana utaratibu wa kwenda kugonga mihuri ya mizigo inayotoka Dar es Salaam kwamba iko on transit na nilitoa evidence (ushahidi) zote mpaka yule dereva aliyekuwa anabeba mizigo,” alisema.

Akitoa maagizo kwa kamishana mkuu mpya, Rais Magufuli alisema tayari ameshamtumia meseji za malalamiko ya wafanyabiashara.

“Sisi tunataka kodi yetu ipatimakane, hakuna nchi duniani iambayo ita survive (itaishi) bila kodi, survival ya nchi ni kodi, mishahara ya wanajeshi wote hawa ni kodi. Niache kuwalipa mishahara hawa si nitawakuta pale Ikulu wamesimama nitawajibu nini?” alihoji.

“Usiogope kuwafukuza, wengine shika peleka mahakamani. Kama kuna wafanyakazi 1,000, 100, 200 wakafukuzwa na kwenda mahakamani, that’s fine (hiyo ni sawa).”

Advertisement