Mkenya aeleza jinsi alivyopata tuzo ya ualimu bora duniani

Mwalimu Peter Tabichi kutoka Kenya akinyanyuliwa mikono baada ya kushinda dola milioni moja za tuzo ya mwalimu bora Dubai, Falme za Kiarabu, Jumapili Machi 24, 2019. Picha na AFP

Muktasari:

  • Ni mtawa aliyewashinda washiriki wengine 10,000 kutoka nchi 179 duniani

Nairobi, Kenya. Mwalimu wa masomo ya hesabu na fizikia Peter Tabichi wa kijiji kilichopo eneo la Bonde la Ufa Kenya ameshinda tuzo ya mwalimu bora duniani 2019 na kuibuka na kitita cha dola milioni moja.

Tabichi, kwa kawaida yake hutoa asilimia 80 ya mshahara wake wa mwezi kwa watu masikini, alipata tuzo hiyo katika sherehe iliyofanyika siku ya Jumamosi Dubai.

Pia mwalimu huyo anayefundisha Sekondari ya Keriko iliyopo mjini Nakuru, huwa anasaidia wanafunzi wake wasiojiweza kununua sare za shule na vitabu.

“Kila siku barani Afrika tunafungua ukurasa mpya wa maisha. Tuzo hii hainitambui mimi bali inawatambua vijana wa bara hili. Nipo hapa kwa sababu ya kile ambacho wanafunzi wangu wamefanikiwa katika maisha yao,” alisema Tabishi.

‘‘Uaminifu ,uwezo wangu ndio hasa chanzo cha kuwa mshindi wa tuzo hii’’alisema

“Tuzo hii inawapa wao fursa. Inauambia ulimwengu kwamba wanaweza kufanya kitu chochote,” aliongeza mwalimu huyo baada ya kuwashinda walimu wengine tisa kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu waliofanikiwa kufika fainali kuwania tuzo hiyo ya mwalimu bora.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alimpongeza mwalimu huyo akimwambia kwamba ‘’historia yako ni stori kwa Afrika, hili ni jambo zuri kwetu na kwako pia’’

“ La muhimu si pesa,” alisema Tabichi, ambaye wanafunzi wake wengi wanatoka katika familia masikini. Wengi ni yatima wengine wamepoteza mzazi mmoja.

Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 36-anataka kuwa mfano na kusaidia kuinua sayansi si kwa Kenya tu bali kote barani Afrika.

“ Vijana wa Afrika hawatabakizwa nyuma na matarajio ya chini’’. Afrika itaweza kutoa wanasayansi, wahandisi, wajasiliamali, ambao majina yao yatakuwa miongoni mwa watu maarufu katika kila kona ya dunia. Na wasichana watakuwa sehemu kubwa ya historia hii .”

Tuzo hiyo ilitolewa kwenye shindano lililoandaliwa na Wakfu wa Varkey , ilitolewa kwa mtawa huyo wa shirika la Mtakatifu Francisco, la Katoliki lililoanzishwa na Mt. Francis wa Assisi katika karne ya 13.

Mshindi wa tuzo hiyo mwaka jana alikuwa ni mwalimu wa sanaa kutoka kaskazini mwa London Andria Zafirakou na miongoni mwa walimu wa kwanza mwaka huu ni Andrew Moffat.

Mwasisi wa tuzo hiyo , Sunny Varkey, alisema anaimani tuzo ya Tabichi itawapa msukumo walimu wote duniani.