Muziki wa reggae waongezwa katika urithi wa dunia

Muktasari:

  • Muziki huo ulijulikana zaidi wakati wa mapambano ya ukombozi barani Afrika hasa baada ya nguli wa muziki huo, Bob Marley kutumbuiza wakati wa uhuru wa Zimbabwe.



Muziki wa reggae wa nchini Jamaica, ambao ni wa watu wanaokandamizwa na ambao Bob Marley aliuingiza katika anga la dunia, umepewa nafasi katika orodha ya Umoja wa Mataifa ya urithi wa dunia wa utamaduni.
Unesco, chombo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na utamaduni na sayansi, kiliuongeza muziki huo katika orodha ua "urithi wa dunia usioshikika" na ambao unastahili kulindwa na kutangazwa, pamoja na vitu vingine kadhaa vya utamaduni duniani.
"Hii ni siku ya kihistoria. Tuna furaha sana," alisema Waziri wa Utamaduni wa Jamaica, Olivia Grange wakati alipozungumza kwa simu kutokea Mauritius ambako suala hilo lilitangazwa.
"Kokote uendake ukisema unatoka Jamaica, wanakujibu 'Bob Marley,'" alisema Grange, akiongeza kuwa kutambuliwa kwa muziki huo "kunathibitisha umuhimu wa utamaduni wetu na muziki wetu, ambao maudhui na ujumbe wake ni upendo mmoja, mshikamano na amani.'"
Unesco ilisema kuwa wakati reggae ilianza kama muziki wa "sauti ya wanaokandamizwa" sasa "unachezwa na kupendwa na watu wa aina tofauti katika jamii, ikiwa ni pamoja na jinsia tofauti, kabila na vikundi vya kidini."
Mchango wake katika anga za kimataifa katika masuala ya haki, mapambano, upendo na utu unaonyesha umuhimu wa mabadilikko ambayo umekuwa ukipitia, kisiasa, kiroho na kihisia, ilisema taarifa ya Unesco.
Unesco inajulikana kwa orodha yake maarufu ya Urithi wa Dunia wa Asili na Utamaduni, ambao unahusisha vitu kama miamba ya Grand Canyon, ukuta wa China wa Great Wall na mji wa kizamani wa Yerusalem.