Nyota wa muziki wa R&B Chris Brown ahojiwa Ufaransa kwa tuhuma za kubaka

Tuesday January 22 2019

 

Paris. Nyota wa muziki wa R&B wa Marekani, Chris Brown anahojiwa na polisi wa Paris baada ya kutuhumiwa kubaka, watu walio katika duru za kipolisi wameiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
Mwanamke mmoja amemtuhumu Brown, pamoja na baunsa wake na rafiki, kuwa alimbaka katika hoteli ya Mandarin Oriental jijini Paris usiku wa kuamkia Jumatano wiki iliyopita, kwa mujibu wa mtoa habari huyo.
Gazeti la Le Figaro liliripoti mapema wiki hii kuwa nyota huyo mwenye mazonge na ambaye ana historia ya kufanya vurugu, alikuwa katika mji huo mkuu wa Ufaransa kuhudhuria maonyesho ya mavazi ya haute couture.
Haute couture ni maonyesho ya mavazi ya bei mbaya, yanayohusisha vitambaa visivyo vya kawaida na ambayo mavazi yake hushonwa kwa mkono na kwa uangalifu mkubwa.
Brown alipata umaarufu duniani baada ya kibao chake cha kwanza cha "Run It" kushika nafasi ya kwanza katika chati ya nyimbo ya Bilboard, akiwa ni wa pili baada ya rapa  P.Diddy kufanya hivyo mwaka 1997.
Albamu yake ya pili ya  Exclusive aliyoitoa mwaka 2007 pia ilitikisa dunia baada ya kibao cha "Kiss Kiss" kushika nafasi ya kwanza katika vibao 100.

Advertisement