Ubelgiji kumpokea Gbagbo

Saturday January 19 2019

 

Brussels, Ubelgiji. Serikali ya Ubelgiji imesema ipo tayari kumpokea na kumpa hifadhi aliyekuwa rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo aliyefutiwa mashtaka hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kuamuru aachiliwe huru.

Hata hivyo, mwendesha mashitaka wa ICC Fatou Bensouda juzi alikataa rufaa dhidi ya uamuzi wa kuachiliwa huru siku moja baada ya ICC kumfutia mashtaka akiwa na msaidizi wake, Charles Ble Goude na kuamuru waachiliwe huru.

Waziri wa vijana ambaye pia ni naibu msemaji wa chama cha RHDP, Mamadou Toure alisema Serikali ya Ubelgiji imesema ipo tayari kumpokea Gbagbo lakini haitakubali kumpokea Ble Goude.

“ Gbagbo ni mwanasiasa na ambacho tunafahamu ni kwamba atakuwa huko Ubelgiji. Serikali ya Ubelgiji na imethibitisha dhahiri kuwa itampokea iwapo atakwenda. Sasa hatua ya Gbagbo kurejea nchini mwake ni jambo ambalo litajadiliwa kwa undani kati yake na Rais Allassan Ouattara,” alisema.

Bensouda, aliomba Gbagbo na Ble Goude kuendelea kushikiliwa gerezani wakati anaendelea kupata na kutathmini sababu za majaji kuwaachilia huru.

Msemaji wa ICC, Fadi El Abdallah alisema uamuzi wa kitengo cha rufaa cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kuendelea kumzuia Gbagbo na Ble Goude ulichukuliwa na majaji watatu kati ya watano.

Kitengo cha rufaa kilibaini kwamba kuna sababu za kipekee za kuendelea kuwashikilia viongozi hao kwa kusubiri uamuzi kuhusu rufaa ya mwendesha mashtaka.

“Kuzuiliwa kwao ni kwa muda, kitengo cha rufaa cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,” kilisema.

Advertisement