Abiria wa nchi 33 wafariki na ndege ya Ethiopia

Muktasari:

  • Ndege hiyo ilipoteza mawasiliano dakika sita baada ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa, Ethiopia kuelekea Nairobi, Kenya.

Addis Ababa, Ethiopia. Taarifa ya Shirika la Ndege la Ethiopia imesema kuwa abiria kutoka nchi 33 waliosafiri kwenye ndege ya shirika hilo iliyopata ajali wote wamefariki.

Msemaji wa kampuni hiyo, Asrat Begashaw, amesema ndege ya kampuni hiyo aina ya Boeing 737- 8 Max iliyokuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi imeanguka Jumapili asubuhi.

Taarifa hiyo imefafanua kwamba walipoteza mawasiliano na ndege iliyopata ajali dakika sita baada ya kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole mjini Addis Ababa.

Msemaji huyo alisema wasafiri 149 na wahudumu wanane waliokuwemo ndani ya ndege hiyo hakuna hata mmoja aliyenusurika, wote wamekufa, aliliambia Shirika la Habari la Kitaifa la Ethiopia.

Kampuni hiyo inasema imeanzisha kituo cha kupata taarifa kuhusu familia na marafiki za watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abey Ahmed imetoa taarifa ikitoa rambirambi kwa familia za waliowapoteza wapendwa wao katika jali hiyo.

Kituo cha ufuatiliaji wa safari za ndege kwa kwa saa 24 kimekuwa kikitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu ajali hiyo.

Ndege hiyo ambayo ilitarajiwa Nairobi iliondoka Uwanja wa Ndege wa Bole mjini Addis Ababa saa 2:38 asubuhi kwa saa za Ethiopia lakini ikapoteza mawasiliano saa 2:44 asubuhi kwa saa za Ehiopia.

Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Airways, Sebastian Mikosz ametuma salamu zake za rambirambi kupitia ukurasa wa Twitter kwa familia na wale waliowapoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo.