Aliyekuwa msafara wa rais, akamatwa akijaribu kuingiza kimagendo maboksi 10,000 za sigara

Muktasari:

Nchini Taiwan, msafiri anaruhusiwa kubeba maboksi matano ya sigara anapotoka nje ya nchi, na moja kati ya hayo linaweza kutozwa kodi.

Kiongozi wa usalama wa raia nchini Taiwan amejiuzulu baada ya wakala ambaye alikuwa kwenye msafara wa Rais Tsai Ing-wen nje ya nchi, kukamatwa akijaribu kuingiza kimagendo karibu katoni 10,000 za sigara.

Kiongozi wa Ofisi ya Usalama wa Taifa (NSB), Peng Sheng-chu aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwake Alhamisi kwa lengo la kuwajibika, ofisi ya rais ilisema.

Kashfa hiyo inamuhusu wakala aliyekuwa kwenye msafara wa Tsai ambaye alijaribu kuingiza maboksi 9,800 ya sigara kwa kupitia eneo la watu muhimu (VIP) wakati wakirejea kutoka katika ziara ya kikazi ya visiwa vya Caribbea jana Jumatatu, mamlaka ya forodha ilisema.

Wakala huyo, ambaye aliagiza sigara hizo kwa njia ya mawasiliano ya mtandao kabla ya kuondoka Taiwan, alizihifadhi kwenye ghala lililopo uwanja wa ndege, na baadaye kujaribu kuziingiza nchini humo kwa kupitia sehemu ya VIP, kwa mujibu wa mbunge wa upinzani ambaye alizitaarifu mamlaka kuhusu suala hilo na vyombo vya habari.

Ofisi ya Tsai ilisema rais "alistushwa na amekasirishwa" na kashfa hiyo na ameagiza uchunguzi ufanyike.

Rais pia aliandika taarifa yake kwenye ukurasa wa Facebook jana akikubaliana na ukosoaji wa wananchi.

"Tutaangalia na kupitia suala hilo kuzuia kashfa kama hiyo isitokee," aliandika Tsai, ambaye mwakani ataomba kuongoza nchi kwa kipindi cha pili.

Mamlaka za Taiwan zimeweka kiwango cha ukubwa wa mizigo ambayo wasafiri wanatakiwa kubeba ambacho ni katoni tano za sigara-- na ni moja tu ambayo inaweza kutozwa kodi.

Kashfa hiyo ilibainika baada ya mamlaka kupokea taarifa kutoka kwa mbunge wa upinzani, Huang Kuo-chang.

Sigara hizo zina thamani ya zaidi ya dola 200,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh430 milioni za Kitanzania), kwa mujibu wa Huang.