Bobi Wine atangaza kuwania urais Uganda mwaka 2021

Muktasari:

Bobi Wine ambaye ni mbunge wa Kyadondo mashariki nchini Uganda amesema atawania nafasi ya urais kwa niaba ya wananchi wa Uganda kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2021.

Kampala, Uganda.  Mbunge wa Kyadondo nchini Uganda, Robert Kyagulani  maarufu Bobi Wine ametangaza kuwania urais wa nchi hiyo mwaka 2021.

Kauli ya mwanamuziki huyo ni ishara kuwa atapambana na rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni anayeliongoza Taifa hilo kwa miaka 33 sasa.

Februari, 2019 chama tawala Uganda  cha National Resistance Movement (NRM) kilimpitisha Museveni  kuwania urais mwaka 2021.

Hatua hiyo ya NRM ilitangulia na uamuzi uliofanywa mwaka 2017 na wabunge wa Uganda waliopitisha mabadiliko ya katiba ya kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75 ya kuwania urais na kumpa nafasi Museveni.

Katika mahojiano na kituo cha matangazo  cha ‘The Associated Press’ Bob Wine amesema atapambana na Museveni kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

“Nitapambana na Rais Museveni kwa niaba ya watu, ”amesema Bobi Wine.