Bobi Wine sasa ataka Marekani isitishe msaada kwa Uganda

Wednesday September 12 2018

 

Washington, Marekani. Mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ambaye kukamatwa kwake na kuwekwa kizuizini mwezi uliopita kuliibua kilio kimataifa, ameitaka Marekani kuacha kuisaidia Uganda kijeshi.
Katika mahojiano maalumu na shirika la habari la Al Jazeera yakiwa ya kwanza kurushwa kwenye televisheni tangu alipopatiwa matibabu Marekani, Mbunge huyo wa Kyadondo Mashariki mwenye umri wa miaka 36, alisema serikali ya Uganda inatumia msaada wa Marekani kukandamiza watu.
Akizungumza katika kipindi cha 'Talk to Al Jazeera', Kyagulanyi alilitaka Bunge la Congress kusitisha msaada wa dola za Marekani 800milioni kwa jeshi la Ugandan akidai kuwa aliteswa akiwa kizuizini Agosti.
"Ni muhimu hususan kwa walipakodi wa Marekani kujua kwamba msaada mkubwa tunaopata kwa ajili ya jeshi ukweli unatumika kukandamiza na kutesa raia wa Uganda, bunduki iliyomuua dereva wangu ambayo inawezekana kabisa ingeniua ni ya Marekani," alisema.
Mbunge huyo na mkosoaji mkubwa wa Rais Yoweri Museveni aliwasili Marekani Septemba Mosi kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kudai aliteswa na vikosi vya usalama vya Uganda, dai ambalo serikali imekanusha lakini ikaahidi kufanyia uchunguzi.
Kyagulanyi alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini katika kile kilichodaiwa alihusika katika kupigwa mawe msafara wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arua Agosti 13.
Siku hiyohiyo baadaye Kyagulanyi aliandika kwenye Twitter: "Polisi wamemuua kwa kumpiga risasi dereva wangu wakidhani waliyemuua ni mimi."

Advertisement