Boeing Max 8 ilivyopoteza watu muhimu

Jaribu kufikiri mtoto wako ambaye ni mtumishi wa Umoja wa Mataifa (UN), anakuaga anakwenda kuhudhuria mkutano wa kimataifa akiwa na afya njema, bashasha na furaha tele.

Baada ya muda mfupi unapata taarifa ya ajali ya ndege ambayo yeye alikuwa ni miongoni mwa abiria na inaelezwa kuwa hakuna abiria wala mhudumu wa ndege hiyo aliyenusurika.

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Adrian Toole, baba wa Joanna Toole mmoja wa Waingereza saba waliofariki dunia katika ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines iliyotokea juzi asubuhi nchini Ethiopia.

Katika ajali hiyo watu 157 kutoka mataifa mbalimbali waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo na wakiwamo wahudumu wake, walipoteza maisha.

Joanna (36) alikuwa safarini kwenda jijini Nairobi, Kenya kuhudhuria mktano wa mazingira.

Toole alilieleza Shirika la habari la Sky News kuwa, amepoteza binti aliyekuwa akijitambua, mtetezi wa mazingira, haki za wanyama na aliyekuwa msaada katika jamii.

“Kwa muda mrefu amekuwa akihangaika huku na kule kwa ndege akiwa katika harakati za kutekeleza majukumu yake. Binafsi nilikuwa nikiona hiyo ni hatari kwake, lakini sikuwa

na namna nyingine kwa kuwa alifanya hivyo kutimiza wajibu na ni jambo alilolifurahia,” anasema Toole.

Anasema “harakati za mapambano ya haki za wanyama na mazingira kwake ilikuwa ni zaidi ya kazi. Ni jambo lililokuwa katika mishipa ya damu yake tangu akiwa mtoto, usingeweza kumtenganisha nalo wakati wowote alikwenda mahali popote duniani kwa ajili hiyo”.

Kwa mujibu wa baba huyo, binti yake amekuwa akijishughulisha na harakati hizo kwa miaka 15 na kuzunguuka sehemu mbalimbali duniani akipigania haki za wanyama na mazingira.

Katika moja ya ujumbe wake alioweka kwenye mtandao wa Twitter, Joanna alijipambanua kuwa mtu anayesikia fahari kuwa sehemu ya mapambano ya kulinda bahari na mpenda amani ya dunia.

“Hakuwa mtu mwenye hofu, alipenda kufanya kazi za kutetea haki za wanyama, amezunguuka sehemu mbalimbali duniani kwa zaidi ya miaka 15 akitimiza jukumu hilo, nilijivunia kuwa naye, lakini sasa najaribu kufikiria maisha bila yeye yatakuwaje,” anasema.

Joanna amekuwa akifanya kazi na UN tangu mwaka 2016 akiishi Rome Italia kabla ya hivi karibuni kurejea nchini Uingereza.

Mwenginbe aliyepoteza maisha katika ndege hiyo ni Joseph Waithaka, Mkenya aliyekuwa na uraia pia wa Uingereza aliyeishi nchini humo kwa zaidi ya miaka 10 kisha kurejea Kenya mwaka 2015.

Mara kwa mara Waithaka alikuwa akimtembelea mke na watoto wake nchini Uingereza wanaoishi katika mji wa Hull na safari hii alikuwa akirejea Kenya kutokea nchini humo kupitia Ethiopia.

Mmoja wa watoto wake, Ben Kuria anasema “baba yetu alikuwa mkarimu mwenye moyo wenye kuguswa na wengine, aliyependa kusaidia watu kutambua fursa mbalimbali”.

“Alikuwa na uwezo wa kueleza habari yenye kuwaamsha na kuwahamasisha vijana waliokata tamaa.

“Ni baba bora tuliyemhitaji, alitusimamia kuhakikisha tunajikita katika kupata elimu. Kwa hakika alikuwa ni kama mzizi uliotushikilia watoto wake,” anasema.

Ilivyopoteza wataalamu

Taasisi mbalimbali zimetoa taarifa za wale wanaozihusu waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo.

Miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na Mwakilishi wa Kamishana wa Wakimbizi wa UN, na mwajiriwa mmoja wa Benki ya dunia.

Kwa mujibu wa orodha ya baadhi ya waliotambuliwa kuwamo katika ndege hiyo, yupo pia Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya misaada ya kibinadamu ya Tamarind Group, Jonathan Seex.

Mbunge kutoka chama cha Slovak National Party cha nchini Slovakia, Anton Hrnko anasema mke wake Blanka, binti yake Michala na mtoto wake wa kiume Martin ni miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo.

Pia, wamo wanakikundi watatu wa kikundi cha misaada kwa Afrika kutoka nchini Italia cha Tremila ambapo rais wake Carlo Spini, anasema miongoni mwao ni mke wake Gabriella Viggiani na mweka hazina wao, Matteo Ravasio ambao pia ni sehemu ya raia wanane wa nchi hiyo.

Jukwaa la Vijana wa Afrika walioko Ughaibuni (Ulaya), linasema Mwenyekiti mwenza wa jukwaa hilo, Karim Saafi alikuwa abiria katika ndege hiyo akiwawakilisha katika mkutano wao na Umoja wa Afrika mjini Nairobi, Kenya.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Carleton cha mjini Ottawa, Canada anasema miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na Profesa Pius Adesamni kutoka chuoni hapo.

Klabu ya Sofapaka inasema Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya, Hussein Swaleh ni miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Nigeria, inasema mwanadiplomasia wake Abiodun Oluremi Bashua aliyewahi kufanya kazi Iran na Ivory Coast ni miongoni mwa waliopoteza maisha.

Navyo vyombo vya habari vya Italia vimeripoti kuwa katika ndege hiyo kulikuwa na madaktari watatu wenye umri kati ya miaka 30 na 40 waliokuwa wakifanya kazi katika hospitali ya Linz.

Nalo shirika la Save the Children linasema mmoja wa washauri wake katika mambo ya dharura, Tamirat Mulu Demessie ni miongoni mwa waliokufa.

Ubalozi wa Urusi nchini Ethiopia unasema watalii watatu kutoka nchini mwake, Yekaterina Polyakova, Alexander Polyakov na Sergei Vyalikov nao wamepoteza maisha katika ajali hiyo.

Obama, May wawalilia

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, katika salamu zake za rambirambi anasema ameguswa na ajali hiyo iliyogharimu maisha ya watu wengi.

“Katika kipindi hiki kigumu, nawapa pole ndugu, familia na marafiki wa raia wote wa Uingereza waliofariki dunia katika ajali hiyo na wengine waliotharika na tukio hilo,” alisema.

Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama aliandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa yeye na mke wake, Michelle wanatoa pole kwa walioguswa na ajali hiyo.