Bunge Liberia lamfunga waziri kwa kukashfu wabunge

Friday September 14 2018

 

Monrovia, Liberia.  Uamuzi huo uliofikiwa katika mjadala wa kisheria wa wabunge, siyo hukumu ya kesi mahakamani ulitosha kumtia hatiani na kumfunga kwa siku mbili Naibu Waziri wa Habari, Eugene Fahngon kutokana na tabia mbaya.
Naibu waziri huyo alitumia usiku wake wa kwanza jela Jumatano na alitarajiwa kutolewa jana.
Anatumikia kifungo hicho cha siku mbili katika Gereza Kuu la Monrovia baada ya Bunge Dogo kumpata na hatia ya kuwakashfu wabunge wawili wa Baraza la Wawakilishi, shirika la habari la BBC limeripoti.
Katika kile kilichoelezwa ni mjadala mgumu, waziri Fahngon aliheshimu mwaliko kutoka kwa watunga sheria ili afafanue mzozo uliosababisha yeye kutoa kashfa dhidi ya wabunge.
Lakini alipofika mbele ya Bunge alisema hakuwa na nia ya kuelezea maudhui yaliyosambaa na kwamba watungasheria hao wanaweza kuchukua hatua kutokana na maoni hayo kama wanavyotaka.
Spika wa Bunge, Bhofal Chambers alitangaza hukumu hiyo na muda mfupi baadae alipigwa pingu na kupelekwa gerezani. Alisema Bunge lilikuwa linaifahamisha serikali kwamba waziri huyo aliyekosea hakuwa nyenzo ya maana serikalini.
Vituo vya radio katika nchi za Afrika Magharibi pia vilitangaza mara kwa mara matusi aliyotoa waziri huyo. Serikali ya Liberi chini ya Rais George Weah haikutoa maoni yake rasmi juu ya tukio hilo.
Liberia ina Bunge la Juu ambalo linaitwa Seneti. Hadi ulipofanyika uchaguzi mkuu mapema mwaka huu, Weah alikuwa Seneta katika Kaunti ya Montserrado.

Advertisement