China yasimamisha matumizi ya ndege za Boeing 737 max 8

Muktasari:

  • Ni baada ya kutokea ajali mbili za Indonesia na Ethiopia

China. China imesimamisha mashirika yake ya ndani kutumia ndege aina ya Boeing 737 Max 8 kufuatia ajali mbili za ndege hiyo zilizotokea Ethiopia na Indonesia.

Hatua hiyo imefikia baada ya kutokea ajali iliyosababishwa na ndege aina hizo katika nchi za Ethiopia na Indonesia.

Serikali hiyo ilikumbushia ajali ya kwanza iliyohusisha ndege hizo ilitokea Jakarta, Indonesia ambapo iliua watu 189.

Jana taarifa ya Shirika la Ndege la Ethiopia imesema kuwa abiria kutoka nchi 33 waliosafiri kwenye ndege ya shirika hilo iliyopata ajali wote wamefariki.

Msemaji wa kampuni hiyo, Asrat Begashaw, amesema ndege ya kampuni hiyo aina ya Boeing 737- 8 Max iliyokuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi imeanguka Jumapili asubuhi.

Taarifa hiyo imefafanua kwamba walipoteza mawasiliano na ndege iliyopata ajali dakika sita baada ya kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole mjini Addis Ababa.

Msemaji huyo alisema wasafiri 149 na wahudumu wanane waliokuwemo ndani ya ndege hiyo hakuna hata mmoja aliyenusurika, wote wamekufa, aliliambia Shirika la Habari la Kitaifa la Ethiopia.

Kampuni hiyo inasema imeanzisha kituo cha kupata taarifa kuhusu familia na marafiki za watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abey Ahmed imetuma salamu za rambirambi kwa familia za waliowapoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.

Kituo cha ufuatiliaji wa safari za ndege kwa kwa saa 24 kimekuwa kikitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu ajali hiyo.

Ndege hiyo ambayo ilitarajiwa Nairobi iliondoka Uwanja wa Ndege wa Bole mjini Addis Ababa saa 2:38 asubuhi kwa saa za Ethiopia lakini ikapoteza mawasiliano saa 2:44 asubuhi kwa saa za Ethiopia.