Chuo Kikuu kutoajiri maprofesaa wavuta sigara

Muktasari:

  • Uamuzi huo umechukuliwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti uvutaji sigara kabla ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika Tokyo

Chuo kikuu cha nchini Japan kimeacha kuajiri maprofesa na walimu wanaovuta sigara, ofisa wa chuo hicho amesema leo Jumanne, ikiwa ni mikakati ya nchi kupambana na uvutaji sigara kabla ya kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020.
Msemaji wa Chuo Kikuu cha Nagasaki, Yusuke Takakura ameiambia AFP kuwa wamesimamisha "kuajiri walimu wanaovuta sigara", ingawa waombaji wanaoahidi kuachana na tabia hiyo kabla ya kuajiriwa, watapewa ajira.
Chuo hicho pia kitapiga marufuku uvutaji kwenye maeneo yake kuanzia Agosti, na itafungua kliniki kwa ajili ya wale watakaoshindwa kuacha uvutaji, alisema Takakura.
"Tumefikia uamuzi kwamba wavutaji hawafai kwa sekta ya elimu," alisema na kuongeza kuwa chuo hicho kiliomba ushauri wa kisheria na hakidhani kuwa uamuzi huo unakiuka sheria ya ubaguzi.
Vyombo vya habari vilisema hii ni mara ya kwanza kwa chuo kinachomilikiwa na Serikali kuanzisha masharti kama hayo katika ajira na uamuzi huo umekuja baada ya Japan kupitisha sheria ngumu za uvutaji kabla ya Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto mwakani.
Kwa muda mrefu, Japan imekuwa ikijitenga na mataifa yaliyoendelea na inachukuliwa kama paradiso ya wavutaji kwa kuwa uvutaji sigara unaruhusiwa katika migahawa mingi na baa.
Sheria mpya zimepiga marufuku uvutaji sigara kwenye migahawa katika jiji la Tokyo bila ya kujali ukubwa wake. Migahawa inaweza kutenga chumba tofauti kwa ajili ya wavutaji, lakini wateja hawawezi kula wala kunywa kwenye eneo hilo.
Pia uvutaji umepigwa marufuku kabisa katika majengo ya shule za chekechea hadi elimu ya juu ya sekondari, ingawa sehemu inaweza kutengwa nje ya vyuo vikuu na hospitali. AFP