Facebook yafuta ukurasa wa mwanasiasa wa siasa kali

Muktasari:

Mtandao huo wa kijamii umesema mwanasiasa huyo amekiuka miongozo ya matumizi inayokataza lugha za chuki na kuhamasisha vurugu dhidi ya makundi ya kijamii

Kampuni inayoendesha mtandao wa Facebook jana iliiondoa akaunti ya mwanasiasa wa Uingereza mwenye mrengo wa kulia, Tommy Robinson kwa kukiuka viwango vilivyowekwa kwa mitandao ya wengi na kuonyeha tabia nyingine ambazo zimezuiwa.
kampuni hiyo kubwa ya Marekani ilisema Robinson, mwanasiasa mtata ambaye alianzisha chama cha kupambana na Uislamu nchini Uingerezaa (EDL), alitumia mtandao huo kushirikisha wengine maneno yanayoshusha utu na kuhamasisha vurugu dhidi ya Waislamu.
Kampuni hiyo ilisema inafunga ukurasa wa mwanasiasa huyo wa Facebook na Instagram kwa sababu miongozo yake inakataza "lugha za chuki ambazo zina mazingira ya kutisha na kuondoa makundi fulani ya watu".
"Ukurasa wa Tommy Robinson wa Facebook umekuwa ukikiuka mara kwa mara miongozo hii, ikituma vitu ambavyo vinashusha ubinadamu na kuhamasisha vurugu dhidi ya Waislamu," kampuni hiyo ilisema katika taarifa yake.
"Pia ameonyesha tabia yake kwa njia ambayo inakiuka sera zetu kuhusu chuki dhidi ya makundi.
"Huu si uamuzi tunaochukulia kirahisi, lakini watu na taasisi wanaoshambulia wengine kwa misingi ya wao ni nani, hawana nafasi kwenye Facebook na Instagram."
Robinson, ambaye jina lake halisi ni Stephen Yaxley-Lennon -- jina alilochukua kutoka kwa shabiki maarufu mkorofi wa soka kutoka nyumbani kwao Luton katikati ya England, ni mbaguzi mkubwa.
Ameshawahi kukutwa na hatia ya matumizi ya dawa za kulevya na pia alifungwa mwaka jana kwa kosa la kurusha matangazo moja kwa moja kwenye mitandao kutoka mahakamani kinyume na masharti ya kuripoti kesi za makundi yaliyoshtakiwa kwa makosa ya mashambulizi ya kingono.