Grace Mugabe alivyoharakisha Robert Mugabe kuachia madaraka Zimbabwe

Thursday November 23 2017Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe.

Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe. 

Harare, Zimbabwe. Mpigania uhuru na mwanamapinduzi mashuhuri barani Afrika Komredi Robert Mugabe ameshusha pazia la uongozi wake baada ya kujiuzulu kama rais wa Zimbabwe na ameacha hatima ya taifa hilo mikononi mwa Jeshi la Ulinzi.

Je, baada ya kuongoza Zimbabwe kwa miaka 37 bado alikuwa na mawazo mapya kichwani? Na katika umri wa miaka 93 bado alikuwa na uwezo wa kuhimili misukosuko ya kiuongozi kimwili na akili timamu? Je, alijiona anapendwa na watu wote milele?

Maswali hayo yanakusudia kujenga nadharia kwa nini kiongozi huyo madhubuti barani Afrika alifikia kutangaza kujiuzulu. Nadharia kubwa inayojengwa katika Makala hii ni namna mkewe Grace alivyochangia kuharakisha shujaa wa ukumbozi wa Zimbabwe kuamua kukaa kando kuanzia juzi.

Kila siku ndani ya nyumba alikuwa akipata shinikizo la kumfukuza yeyote anayewania urais ndani ya chama tawala cha Zanu PF, wiki iliyopita ikulu na majengo yote ya serikali yalikuwa chini ya jeshi, kisha wananchi wakaanza kuandamana mitaani akimtaka ajiuzulu; wabunge nao wakafungua mashtaka bungeni. Halafu Zanu PF ikatangaza kumvua uongozi na kumrejesha makamu wa rais aliyemfukuza.

Hakuwa na njia wala namna isipokuwa kumwandikia barua Spika wa Bunge Jacob Mudenda inayosema: “Mimi Robert Gabriel Mugabe kwa kuzingatia kifungu cha 96 cha Katiba ya Zimbabwe kwa hiari yangu nawasilisha uamuzi wa kujiuzulu... uamuzi unaanza mara moja.”

Mchango wa Grace

Kama Delila wa kwenye Biblia alivyokuwa kiini cha anguko la Samson, Grace, kwa kiasi kikubwa ndiye amechangia anguko hili kutokana na tamaa ya kumrithi mumewe ikiwa atastaafu au kufariki.

Grace ambaye anatofautiana na Mugabe kwa miaka 41, aliwahi kutajwa kuwa mwanasiasa wa uzito mwepesi na mtu ambaye anapenda anasa.

Katika miaka ya hivi karibuni alikuwa akijihusisha zaidi na siasa hadi kufikia kuwa mstari wa mbele kutwaa madaraka ya nchi. Akaanzisha visa. Mjeruhiwa wa kwanza alikuwa Joice Mujuru na mwaka huu alielekeza mashambulizi makali dhidi ya Emmerson Mnangagwa akimshutumu kuwa si mtiifu na baadaye kwamba alipanga njama za kumpindua Magabe.

Oktoba 9, Mugabe alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na akampokonya Mnangagwa ofisi ya waziri wa sheria hali iliyotafsiriwa kwamba makubwa yanakuja na kweli Novemba 6 akafukuzwa kama Makamu wa Rais katika Zanu PF na kama makamu wa Rais wa Zimbabwe.

Hapo ndipo Jeshi lilipoamua kumdhibiti Grace, 52, asiweze kuteuliwa kuwa makamu wa rais – Jumatano ya Novemba 15 likachukua udhibiti wa nchi na kuashiria mwisho wa utawala wa miaka 37 wa Mugabe.

“Mgogoro huu umechochewa zaidi na Grace kwa sababu alikusudia kunyakua madaraka na kumlazimisha Mugabe afukuze watu wengi sana,” amesema Shadrack Gutto ambaye ni mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mwamko wa Kiafrika cha Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.

“Alijifikisha mbali mno. Amefanya mambo mengi yaliyochangia kuharakisha vuguvugu la kumwondoa mumewe madarakani. Jeshi liliona imetosha.”

Mipango ya kisiasa ya Grace ilikuwa inaratibiwa na kundi la vijana ndani ya Zanu PF ambalo lilipewa jina la G40. Kundi hilo lilikuwa likifanya mikakati yake kukabiliana na kundi jingine lenye nguvu liitwalo Team Lacoste lililokuwa likiongozwa na Mnangagwa.

Grace alitumia ushawishi wake kuhakikisha Lacoste linasambaratika na ndiyo sababu ya kumshambulia Mnangagwa kwenye mikutano hadharani hadi akafukuzwa. Kitu ambacho Grace ama alipuuza au hakuwa anajua, Mnangagwa ni veterani wa vita vya ukombozi na amekuwa akiungwa mkono na maveterani pamoja na jeshi.

Hii ndiyo sababu mara baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa nchi, kundi la Grace ambalo linajumuisha baadhi ya mawaziri limekuwa shabaha namba moja ya maofisa wa jeshi ambao walitangaza katika TV kupitia shirika la utangazaji la ZBC alfajiri ya Jumatano kwamba watawafikisha kwenye vyombo vya sheria “wahalifu” walioko kando ya Mugabe.

Jeshi la Zimbabwe linaona kwamba bado lina haki ya kuwa na rais watakayemwidhinisha. Waliona ni busara kuchukua hatua sasa kabla ya Grace kuteuliwa kuwa makamu wa rais katika mkutano mkuu mwezi ujao.

Alikotokea Grace

Historia inaonyesha Grace Ntombizodwa alizaliwa Julai 23, 1965 katika kijiji cha Benoni, Afrika Kusini akiwa mtoto wa nne kati ya watano. Wazazi wake walikuwa wahamiaji. Mwaka 1970 alirudi Zimbabwe (Rhodesia ya zamani) na mama yake Idah Marufu na wakawa wanaishi Chivhu. Alisoma shule ya msingi ya Chivhu na baadaye shule ya sekondari ya Kriste Mambo, Manicaland.

Aliolewa na rubani wa ndege za jeshi Stanley Goreraza ambaye walizaa mtoto mwaka 1984 aliyepewa jina la Russell. Grace alikuwa katibu muhtasi katika ofisi ya Mugabe na hali akiwa bado katika ndoa yake mwaka 1987 alianzisha uhusiano na “mzee” na wakazaa watoto wawili Bona na Robert Peter, Jr.

Baada ya mkewe wa kwanza, Sally Hayfron kufariki dunia mwaka 1992, Mugabe aliamua kumuoa rasmi Grace kwa sherehe kabambe zilizopewa jina la “Harusi ya Karne” mwaka 1996. Wakati wanaoana Grace alikuwa na umri wa miaka 31 ilhali Mugabe alikuwa na miaka 72. Mwaka 1997 walizaa mtoto wa tatu aitwaye Chatunga.

Nje na ndani ya siasa

Kipindi ambacho hakuwa na mpango na siasa alifahamika kwa tabia yake ya kuponda raha, matumizi makubwa ya fedha akinunua majumba Afrika Kusini, kununua mikufu ya alimasi na magari ya kifahari kama Rolls-Royce kwa ajili ya watoto wake, kununua nguo, kukaa kwenye mahoteli ghali, kusafiri sana nje ya nchi na kujihusisha na ufisadi wa ardhi.

Mambo hayo yalisababisha apewe jina la utani la Gucci Grace au DisGrace. Lakini mashabiki wake walimpamba kwa kumwita ‘Dokta Amai’ yaani Dokta Mama na Malikia wa mamalikia.

Mwaka 2014 Grace alijiandikisha kusomea shahada ya kwanza lakini katika mazingira ya kutatanisha miezi mitatu baadaye akatunukiwa shahada ya heshima na Chuo Kikuu cha Zimbabwe, ambako mumewe alikuwa kansela.

Mwaka 2014 akachaguliwa kuwa mkuu wa tawi la wanawake wa chama cha Zanu PF. Hapo akaanzisha kampeni chafu dhidi ya aliyekuwa makamu wa rais Joice Mujuru, ambaye alikuwa na nafasi kubwa ya kumrithi Mugabe. Grace alidai Mujuru alikuwa anafanya njama za kumpindua mumewe hadi makamu huyo akaondolewa na akafukuzwa Zanu PF.

Kampeni za kummaliza Mnangagwa zilizokuwa zikifanywa kwa staili ileile – kwamba hamtii mumewe, anakutana na watu waliofukuzwa Zanu PF na anataka kumpindua Mugabe zimewasababisha majanga

Kwamba wakati Mnangagwa amerejeshwa kwenye chama na kuteuliwa kuongoza Zanu PF, Grace na Mugabe wako kizuizini nyumbani. Zanu PF wametoa taarifa kwamba Mnangagwa ataapishwa kesho kuwa rais kumalizia kipindi kilichosalia hadi 2018.

Advertisement