Hali tete Cameroon

Wednesday September 12 2018

Yaounde, Cameroon. Kamishna mpya wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama eneo la watu wanaozungumza kiingereza nchini Cameroon.
Bachelet amesema hali iliyopo inahitaji kutupiwa jicho haraka kutokana na Serikali kushindwa kuchukua jukumu la kuongoza kuhakikisha unapatikana ufumbuzi katika mgogoro huo.
Mwanamama huyo amezungumzia hali ya uchumi, jamii na athari za hali ya chuki iliyopo kati ya Serikali na makundi ya wanaotaka kujitenga, akishutumu mashambulizi dhidi ya walimu na wanafunzi katika mikoa ya Kusini Magharibi na Kaskazini Magharibi.
Kauli ya Bachelet ilikuwa ni sehemu ya hotuba yake ya ufunguzi katika kikao cha 39 cha Baraza la Haki za Binadamu Septemba 10. Mtangulizi wake Zeid Ra’ad al Hussein mara kadhaa alionyesha kusikitishwa na mgogoro huo na akatoa wito kwa Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka.
Hali ya usalama nchini Cameroon imezorota zaidi katika miezi ya hivi karibuni, huku mapigano yakipamba moto katika mikoa inayoitwa ya wazungumza kiingereza kati ya vikosi vya ulinzi na makundi ya watu wenye silaha na raia wengi wakiathirika na zaidi ya watu 180,000 wakilazimika kukimbia nyumba zao. Nchi hiyo sasa inahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
Shughuli nyingi za kiuchumi katika mikoa hiyo zimekwama. Kutokana na hali isiyotabirika kiusalama, watu wengi wanahofia kulipiziwa kisasi ikiwa watashiriki uchaguzi mkuu wa Rais uliopangwa kufanyika mwezi ujao.

Advertisement