VIDEO: Hili ndilo toleo jipya la Boeing Max iliyoanguka Ethiopia

Ethiopian Airlines ni shirika kubwa la ndege na linaloheshimika Afrika na duniani kote. Kwa sasa ndilo linalotajwa kuongoza kwa usalama wa ndege zake pande mbalimbali za dunia.

Ndege za Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines), zinazofanya safari na kuunganisha mabara yote kila siku, zinaelezwa kuwa hadhi na usalama wake ni wa hali ya juu.

Tangu mwaka 1965 ndege zake zimepata ajali mara 60 huku nyingi zikiwa ni zile zisizo na madhara makubwa kwa binadamu.

Boeing 737 MAX 8

Hata hivyo, wakati hali ikiwa shwari kwa Ethiopian Airlines, ndege za Boeing hususani toleo la 737 ndege zake zimerekodiwa katika ajali kadhaa tangu zilipoanza kuingia sokoni.

Katika kipindi cha miezi 11 kuanzia Mei, 2018 hadi sasa, ndege tatu za Boeing 737 Max zimehusika katika ajali zikimilikiwa na mashirika tofauti.

Boeing Max 8, ni toleo jipya la familia ya ndege zinazotengenezwa na kampuni ya Boeing ya Marekani. Toleo hili jipya lililotoka mwaka 2013.

Ni ndege zenye umbo jembamba, urefu wake ni mita 39.52 na upana kutoka bawa moja hadi jingine ni mita 35.9.

Miongoni mwa sifa za MAX 8 ina uwezo wa kuchukua abiria hadi 215 na kutembea umbali wa kilomita 6,650 angani bila kutua popote.

Gharama za ndege hiyo inauzwa dola110 milioni za Marekani (Sh250 bilioni).

MAX 8 kwa mara kwanza ilianza kutumiwa mwaka 2016 na Shirika la Ndege la Indonesia la Lion Air, lakini ilipata ajali na kuua abiria wote 189, ilielezwa kuwa ilikuwa na matatizo kwenye mfumo wake wa kasi angani katika safari zake nne za mwisho. Wakichunguza maudhui ya data, Mchunguzi Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Usalama wa Usafirishaji ya Indonesia, ambayo inaongoza uchunguzi wa ajali hiyo, Kapteni Nurcahyo Utomo, alisema; “Tunadhani suala hilio ni muhimu kwa sababu kuna zaidi ya ndege 200 za Max duniani.” Wakati hakuna ishara kuwa Max 8 ina tatizo la kimfumo katika usomaji wa kasi yake angani, upya wa ndege hiyo unamaanisha uwezekano wa uwepo wa tatizo lolote unaweza kuwa bado haujajitokeza katika ndege za mashirika mengine.Hata hivyo, tovuti ya kufuatilia safari za ndege ya Flightradar24 ya Sweden ilisema toleo hilo la ndege aina ya MAX 8 limekuwa na hitilafu hiyo tangu ilipoanza kutumiwa.

Shirika la Ethiopian Airline limejiwekea rekodi barani Afrika kwa kuagiza toleo jipya la Being 787 Max 8 ambalo limetoka mwaka 2013. Ilianza kuruka Oktoba mwaka jana.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtandao wa kampuni ya Boeing, Ethiopian Airline wameagiza ndege kama hizo 30.

Familia ya Boeing aina ya MAX ina matoleo maane ambayo ni 7,8,9, na 10. Iliyopata ajali Indonesia na Ethiopia ni toleo la MAX 8.

Ndege yanayotumia MAX ni Norwegian Air, Air China, TUI, Air Canada, United Airlines, American Airlines, Turkish Airlines na Icelandair na FlyDubai.

Hata hivyo, ndani ya muda mfupi tayari ndege hizo zimeripotiwa kuhusika katika ajali kadhaa ya kwanza ikitokea Oktoba 29, 2018 pale Boeing 737 Max mali ya Shirika la Lion Air ilipodondoka katika bahari ya Java, muda mfupi baada ya kuruka kutoka katika jiji la Jakarta, Indonesia. Watu wote 189 waliokuwamo ndani, abiria na wahudumu walipoteza maisha.

Mei 18, 2018 ndege nyingine ya abiria Boeing 737 ilipata ajali na kuuwa watu 112 baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jose Marti mjini Havana, Cuba. Katika ajali hiyo abiria mmoja tu ndiye aliyesalimika

Sasa ni ajali iliyohusisha ndege ya Boeing 737 mali ya Ethiopian Airline iliyodondoka jana, muda mfupi baada ya kuruka kutoka Addis Ababa na kuua watu wote 157 ilipokuwa ikielekea Nairobi, Kenya.

Wakati ajali ya jana ikiingia katika orodha ya ajali za ndege zilizouwa watu wengi Afrika, katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2010 dunia imeshudia ajali nyingi zilizosababisha vifo vya watu wengi.

Ajali kubwa za ndege zilizowahi kuripotiwa katika kipindi cha miaka 10 ni pamoja na iliyotokea Aprili 11, 2018 ambapo ndege ya kijeshi ilidondoka muda mfupi baada ya kuruka kutoka mji mkuu wa Algeria, Algiers. Watu 257 walifariki wakiwamo wahudumu 10 wa ndege hiyo. Wengi wa waliokufa katika ajali hiyo walikuwa askari na familia zao.

Machi 12 2018 watu 71 walipoteza maisha baada ya ndege aina ya Bombardier kupata ajali wakati ikitaka kutua katika mji wa Kathmandu, Nepal. Takriban watu 50 walifariki dunia.

Februari 18, ndege ya abiria ilidondoka katika milima ya Zagros nchini Iran na kuua watu 66 ikiwa ni muda mfupi tangu iliporuka kutoka mjii mkuu wa nchi hiyo Tehran, kwenda mji wa Yasuj.

Ndege ya Urusi ikiwa na abiri 71, Fbruari 11, 2018 ilidondoka na kuuwa watu wote waliokuwamo. Kwa mujibu wa taarifa, ndege hiyo aina ya Antonov An-148 mali ya shirika la Saratov ilikuwa ikitoka katika uwanja wa ndege wa Domodedovo kwenda mji wa Orsk.

Desema 25, 2016 ndege ya kivita ya Urusi ya Tu-154 jet ilipata ajali katika bahari nyeusi na kuuwa watu 92 abiria na wahudumu. Ilipata ajali muda mfupi baada ya kuruka kutoka mji wa Sochi.

Ajali nyingine ni ile iliyotokea Desemna 7, 2016 na kuuwa watu 48 waliokuwamo katika ndege ya PK-66 iliyokuwa ikitoka mji wa Chitral kwenda Islamabad.

Novemba 28, ndege iliyokuwa imebabeba wachezaji na viongozi wa timu ya Chapecoense ya Brazil iliishiwa mafuta na kudondoka karibu na mji wa Medellin, Colombia. Watu 71 walifariki dunia wakiwamo wachezaji. Watu sita walinusurika.

Mei 19, Ufaransa ilithibitisha ndege ya Misri iliyokuwa imepotea kati Cairo na Paris, imepata ajali ikiwa na watu 66.

Ndege nyingine ya Boeing 737-800 mali ya shirika la FlyDubai, ilipata ajali Machi 19, 2016 huko Rostov-on-Don, Urusi na kuuwa watu 62.

Oktoba 31, 2015 ndege ya Airbus A321, ya shirika la ndege la Urusi, Kogalymavia, ilipata ajali katika eneo la Sinai dakika 22 baada ya kuruka kutoka Sharm el-Sheikh, na kuuwa watu wote 224 waliokuwamo ndani.

Juni 30, 2015 ndege ya kijeshi ya Indonesia, Hercules C-130 ilidonda katika eneo la makazi la Medan. Katika taarifa yake, jeshi hilo lilisema watu wote 122 waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo walifariki dunia na wengine 19 waliokuwa ardhini.

Machi 24, 2015 ndege ya abiria ya Ujerumani, Airbus A320 ilipata ajali nchini Ufaransa ikitokea Barcelona, Hispania kwenda Dusseldorf. Watu 148 walipoteza maisha.

Desemba 28, 2014 ndege ya shirika la AirAsia QZ8501 ikitokea Surabaya, Indonesia kwenda Singapore ilipotea katika bahari ya Java ikiwa na watu 162 wakiwamo wahudumu.

Julai 24, 2014 ndege ya Shirika la Algeria AH5017, ilipotea nchini Mali kutokana na hali mbaya ya hewa. Ndege hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na shirika la Hispania la Swiftair, ilikuwa ikielekea Algeria kutokea Ouagadougou, Bukinafaso ikiwa na abiria 116 huku 51 kati yao wakiwa ni raia wa Ufaransa. Wote walifariki duni.

Julai 17, ndege ya Malaysia MH17 ilipata ajali karibu na mji wa Grabove, Ukraine na kuuwa watu 298.