Hong Kong wasitisha safari za ndege

Monday August 12 2019

 

Hong Kong. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hong Kong, China umesitisha safari zote nchini humo kutokana na maandamano yanayoendelea.

Zuio hilo lilotangazwa leo Jumatatu Agosti 12, litazihusisha ndege zote zinazoingia na kutoka katika mji huo wa kibiashara.

Kwa siku nne mfululizo wananchi wa mji wa Hong Kong wamepiga kambi katika uwanja huo kupinga utawala wa nchi hiyo.

Taarifa ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Hong Kong iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilisema kwamba waandamanaji hao wamesababisha shughuli ndani uwanja kukwama.

Kufuatia tangazo hilo Shirika la Ndege la Hong Kong, limewaonya wafanyakazi wake kwamba wanaweza kupoteza ajira iwapo wataunga mkono maandamano hayo.

Tayari hisa za shirika hilo la ndege la Taifa zimeanguka thamani kwa zaidi ya asilimia nne baada ya Beijing kuweka sheria hiyo mpya ya kuwapiga marufuku wafanyakazi wa mashirika ya ndege kushiriki katika maandamano ya mjini Hong Kong.

Advertisement

Wiki iliyopita, shirika hilo lilifuta safari za ndege zaidi ya 150 kutokana na mgomo unaohusishwa na maandamano hayo huku ununuaji wa tiketi ukiwa umepungua tangu harakati za maandamano zianze.

Mapema jana asubuhi polisi mjini Hong Kong walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji ambao kwa zaidi ya miezi mitatu sasa wameingia barabarani kushinikiza sheria za China bara zisitumike visiwani humo.

Polisi pia waliwanyima waandamanaji hao iwaliokuwa wamepanga kufanya mkutano katika kitongoji cha Sham Shui Po. Hata hivyo, licha ya katazo la polisi waandamanaji hao waliendelea.

China imelaani vikali ghasia zinazofanywa na waandamanaji ambao waliwatupia mabomu ya petroli maafisa wa polisi. China imesema vitendo hivyo ni vya kigaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Hong Kong na Macao, Yang Guang aliwaambia waandishi wa habari mjini Beijing kwamba waandamanaji wanatumia zana za hatari kuwashambulia maafisa wa polisi jambo ambalo linakiuka sheria na utaratibu wa kijamii wa Hong Kong.

Hata hivyo, mwanasheria na mwenyekiti wa Taasisi ya Sheria mjini Hong Kong, Lawrence Ma alipendekeza Serikali kuchukua hatua stahili kwa mujibu wa Katiba ili kudhibiti maandamanao hayo.

Mwanasheria huyo alisema “endapo vurugu zitaendelea mjini basi amri ya kutotoka majumbani inawezekana kuwa ndio hatua sahihi.”

Alisema chini ya kifungu hicho cha sheria waandamanaji wanaweza kukabiliwa na adhabu ya vifungo vya maisha jela.

Advertisement