India yahamisha 300,000 kuepuka kimbunga Vayu

Muktasari:

  • Kimbunga Vayu kinatarajiwa kuifikia pwani hiyo kwa kasi ya kilometa 145 hadi 155 kwa saa na kinaweza kwenda hadi kilometa 170 kwa saa.

Mumbai. Inidia imewahamisha watu zaidi ya 300,000 kuepuka kimbunga Vayu kinachotazamiwa kuipiga pwani ya Gujarat leo.

Wataalamu wa hali ya hewa wamesema kimbunga Vayu kinachosafiri kwa upepo ulio katika daraja la kwanza, kinatarajiwa kuifikia pwani hiyo kwa kasi ya kilometa 145 hadi 155 kwa saa na kinaweza kwenda hadi kilometa 170kwa saa.

Serikali ya Jimbo hilo imeanza kuhamisha watu kutoka katika maeneo hatarishi kwenda makazi maalumu.

‘Tumeanza kuhamisha watu katika wilaya za pwani leo asubuhi,” Ofisa wa kuratibu maafu jimbo Gujarat aliieleza Teuters Jumatano Juni 12.

Waziri mkuu wa jimbo hilo, Vijay Rupani alilitaka jeshi la India na Kikosi cha maafa ya nchi hiyo kusaidia shughuli za uokoaji na msaada wa kibinadamu ikiwa kimbunga hicho kitatokea na kusababisha maafa.

Waziri wa mambo ya ndani, Amit Shah pia aliwataka maofisa wa serikali kuhakikisha miundombinu itakayoathirika kama ya umeme, simu na maji kurejeshwa haraka.

Idara ya Hali ya Hewa imesema kimbunga hicho kinaweza kuambatana na mvua za msimu kutokana na upepo huo kusukuma mawingu ya mvua kutoka baharini.

Kimbunga hicho huenda kikaathiri shughuli za bandari ambako pia kuna mitambo ya kusafisha mafuta.

Kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta nchini India kinachomilikiwa na Reliance Industries kiko Gujarat, ingawa ofisa wa kampuni hiyo amesema kimbunga kinatarajiwa kuwa kimepungua nguvu kitakapoifikia mitambo hiyo.

“Lakini ikiwa kutakuwa na mabadiliko, kiwanda kiko tayari kwa dharura,” alisema akikataa kutambulishwa kwa kuwa si msemaji wa kiwanda.

Bandari ya Sikka na Terminals Ltd zinazoshughulika na mafuta ya  Reliance Industries Ltd, zilizuia meli kutia nanga pwani ya magharibi Jumatano, ikiwa ni tahadhari ya kimbunga.

Mwezi Mei Kimbunga Fani, chenye ukubwa wa daraja la nne, kiliua watu 34 mashariki mwa India na kuharibu nyumba nyingi za wakazi.

Mamlaka zilihamisha watu milioni 1.2 kabla ya kimbunga hicho. Kimbunga kikali zaidi kuwahi kutokea India kilitokea mwaka 1999 na kuua watu karibu 10,000 na kusababisha uharibifu wa mabilioni ya dola za marekani.