Iran yakamata meli mbili za Uingereza

Teheran. Jeshi la Kimapinduzi la Iran limesema limekamata manowari yenye bendera ya Uingereza katika lango la bahari la Hormuz baada ya kukiuka sheria za kimataifa za baharini.

Hatua hii inakuja wakati kukiongezeka hali ya wasiwasi katika eneo hilo la bahari.

Uingereza imesema Iran imekamata manowari mbili katika eneo la Ghuba huku waziri wake wa mambo ya nje Jeremy Hunt akionya uwezekano wa hatua kali za kisasi iwapo suala hilo halitashughulikiwa mara moja.

Mmiliki wa manowari ya Mesdar ambayo ni miongoni mwa zilizokamatwa amesema wanajeshi wenye silaha waliingia kwenye meli hiyo kwa muda kabla ya kuiruhusu kuondoka.

Tukio hili linakuja baada ya jana Rais Donald Trump wa Marekani kusisitiza kwamba manowari ya Marekani iliidungua ndege ya Iran isiyokuwa na rubani iliyokuwa ikitishia usalama wa meli na wafanyakazi katika lango hilo la Hormuz.

Hata hivyo Iran ilipinga madai ikisema “huenda Marekani imedungua ndege yake yenyewe kwa bahati mbaya”.