Jacque Maribe arejea Citizen TV

Tuesday December 4 2018

 

Nairobi, Kenya. Mtangazaji maarufu wa Citizen TV, Jacque Maribe amerejeshwa kazini baada ya kupata dhamana katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara mwanamke Monica Kimani.
Vyanzo vya habari vinasema Maribe alikuwa kwenye chumba cha habari kuanzia Jumatatu akiandaa na kupitia taarifa za habari.
Hata hivyo, hataweza kurejea majukumu yake ya kusoma habari kama ilivyoelekezwa na Jaji wa Mahakama Kuu, James Wakiaga alipotoa uamuzi wa kumwachia kwa dhamana.
“Mshtakiwa hataruhusiwa kusoma habari, kutoa maoni au kushiriki katika mahojiano yanayohusu kesi inayomkabili na zaidi hatapaswa kusoma habari katika kipindi ambacho suala hili litakuwa limepangwa kwa ajili ya usikilizwaji."
"Hataruhusiwa kufanya mahojiano mubashara au vinginevyo na upande wowote unaohusiana na kesi ikiwamo familia ya waathirika, wakili, mashahidi wa upande wa mashtaka na Mahakama inayosikiliza,” alisema Wakiaga.
Vyanzo kutoka ndani ya Citizen TV vimesema mwanadada huyo atakuwa akisaidia katika uzalishaji wa habari lakini hatakuwa kwenye TV.
Mara baada ya kukamatwa, mwajiri wake kampuni ya Royal Media Services ilimpa Maribe likizo ya lazima ya miezi mitatu.
Jumanne ya wiki iliyopita aliruhusiwa kuingia kwenye nyumba yake na kutumia gari lake Jumanne baada ya kuwashtaki mwendesha mashtaka mkuu wa umma (DPP) na mkurugenzi wa upelelezi wa makossa ya jinai kwa kutotii maelekezo ya Mahakama.

Advertisement