Jaji afuta utekelezaji wa uamuzi wa Trump kuhusu wahamiaji

Muktasari:

  • Jaji huyo amesemaq uamuzi wa kuzuia wahamiaji ambao hawakupitia katika mipaka rasmi kupata hifadhi, unakiuka sheria za uhamiaji za Marekani.

Jaji wa Marekani jana Ijumaa alifuta hatua ya serikali ya Rais Donald Trump ya kuzuia wahamiaji kuomba ukimbizi hadi wawe wameingia nchi hiyo kwa kupitia katika mipaka rasmi, kwa mujibu wa vyombo vya habari.
Sera hiyo, iliyoanzishwa na Trump mwaka jana, ni moja ya hatua kadhaa ambazo serikali yake imechukua dhidi ya maelfu ya wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao katika siku za karibuni wamekuwa wakijaribu kuingia Marekani wakitokea Mexico na kuomba hifadhi.
Jaji wa serikali ya shirikisho, Randolph Moss, akiwa Washington, aliamua kuwa sera hiyo "ni zaidi ya... mamlaka," iliripoti ABC News.
Moss alisema sera hiyo inakinzana na sheria ndogondogo za uhamiaji za Marekani, ambazo zinaruhusu watu wasio na nyaraka rasmi ambao wako nchini humo kuomba hifadhi hata kama hawakuingia kupitia mipaka rasmi, limeandika gazeti la The Hill.
Awali sera hiyo ilizuiwa na jaji wa San Francisco, uamuzi ambao serikali imekata rufaa.
Sera ya Trump kuhusu uhamiaji imekuwa ikipingwa katika mahakama.
Wiki iliyopita, jaji wa shirikisho kutoka California alitoa amri ya muda ya kuzuia serikali kukataza wahamiaji wengi kupata hifadhi nchini Marekani kama wamepitia Mexico.
Sera hiyo ingezuia waombaji hifadhi wengi kutoka Amerika ya kati kupata ruhusa ya kuingia Marekani kupitia mpaka wa kusini, kwa kuwa wengi wanatokea Mexico.