Jeshi, Mahakama wagomea amri za Rais Duterte

Friday September 14 2018

 

Rais Rodrigo Duterte anakabiliwa na shinikizo kutoka taasisi na jeshi juu ya amri alizotoa akitaka kukamatwa mkosoaji wake mkubwa Antonio Trillanes ambaye amejificha katika jengo la Seneti kwa muda karibu wiki mbili ili kuepuka kukamatwa.
Trillanes ambaye anaendelea kujificha kwa siku ya 11 sasa, alipokea kwa furaha hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Seneti, Jeshi na Mahakama ambapo alisema ilimlazimisha Duterte kulegea na kwamba anasubiri Mahakama itoe uamuzi juu ya uhalali wa amri za Rais huyo kukamata watu.
"Duterte alivuka mipaka na alifanya hesabu vibaya. Alitaka kupanua mipaka ya mamlaka yake ya kiutendaji lakini kwa ujasiri ililazimisha taasisi kumrudisha nyuma. Duterte alilazimika kupoa, walau kwa sasa," Trillanes alisema.
Hivi karibuni kiliibuka 'kimbunga' cha kisiasa kilichochochewa na jaribio la Duterte kutaka kutumia jeshi kumkamata mwanasiasa huyo bila hati yoyote, hali iliyoibua kumbukumbu za matumizi ya sheria za kijeshi miaka ya 1970 wakati jeshi lilijitokeza kuwa uti wa mgongo wa utawala wa kidikteta wa hayati Ferdinand Marcos.
Duterte alijaribu lakini alishindwa kulazimisha jeshi kumweka kizuizini Trillanes na kumfungulia upya mashtaka katika Mahakama ya kijeshi juu ya masuala kadhaa ikiwamo ya mwaka 2007 Trillanes alipoongoza askari katika hoteli za kifahari ili kukemea rushwa katika jeshi na ndani ya Serikali ya Rais wa zamani, Gloria Arroyo.
Rais Duterte alifuta msamaha kwa hoja kwamba Trillanes hakuwa amewasilisha rasmi maombi ya msamaha na alishindwa kujieleza juu ya hatia ya uasi. Nyaraka zilizopo zinaonyesha alifanya yote mawili.
"Ukweli kwamba seneta Trillanes hajakamatwa ni ushindi kwa utawala wa sheria na mchakato wake. Hata hivyo, tunapaswa kuwa macho," alisema Seneta Francis Pangilinan Rais wa chama cha upinzani cha Liberal.
Mwanahistoria wa kijeshi, Jose Antonio Custodio alisema awali jeshi lilionekana kutaka kumkamata Trillanes lakini liliamua vinginevyo baada ya kupokea shutuma kutoka kila kona.
"Ingesababisha mgogoro mkubwa kama jeshi lingemkamata Seneta Trillanes, ungekuwa mwendelezo mbaya sana. Ingefinyanga demokrasia tuliyo nayo nchini," alisema Custodio wakati akizungumzia namna Duterte alivyodhibiti jeshi la polisi ambalo linatekeleza kampeni ya umwagaji damu ya Duterte dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya.

Advertisement