Jeshi, upinzani sasa kugawana uongozi Sudan

Muktasari:

  • Katika makubaliano hayo, pande zote zitashirikiana katika uongozi kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kwenda katika Uchaguzi Mkuu.

Khartoum, Sudan. Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan limesaini makubaliano yatakayowezesha kugawana uongozi na upinzani.

Makubaliano hayo yametiwa saini leo Jumatano Julai 17 na kufuatiwa na sherehe fupi zilizofanyika katika Hoteli ya Corinthia mji mkuu wa Khartoum.

Hatua hiyo imefuatia mazungumzo ya usiku kucha baina ya pande hizo zinazosigana yaliyokuwa yakilenga kumaliza mzozo nchini humo.

Katika makubaliano hayo pande zote zitashirikiana katika uongozi kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kwenda katika Uchaguzi Mkuu.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, uongozi wa kijeshi utakaa madarakani kwa miezi 21 ya kwanza kisha utawala wa kiraia utaidhinishwa katika miezi 18 itakayofuata.

Makubaliano ya pili kuhusu masuala ya Katiba yanatarajiwa kukamilishwa siku ya Ijumaa wiki hii.

Zaidi ya watu 100 wameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya kushinikiza utawala wa kiraia tangu kung’olewa kwa Rais Omar al Bashir Aprili mwaka huu.