Jeshi Nigeria lavamia ofisi za gazeti

Tuesday January 8 2019

 

Abuja, Nigeria. Jeshi la Nigeria limesema limevamia ofisi za gazeti la kila siku la Daily Trust kwa kuhatarisha usalama wa nchi baada ya kuripoti kuhusu operesheni zilizopangwa kutekelezwa na jeshi dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.

"Makala hiyo inahatarisha waziwazi usalama wa wanajeshi," jeshi limesema katika tamko lililotolewa baada ya uvamizi huo.

Uongozi wa gazeti hilo umelaani kitendo hicho na kutaka wafanyakazi wake waachiwe huru.

Jeshi la Nigeria limesema halijapanga kunyamazisha vyombo vya habari, lakini limelazimika kufanya hivyo kwa sababu gazeti hilo lilitoa taarifa ambazo ni za siri.

"Taarifa hiyo imewapa magaidi wa Boko Haram notisi ya mipango yetu na kuwatahadharisha dhidi ya Jeshi la Nigeria na kwa namna hiyo kuhujumu mipango ya kijeshi na kuweka maisha ya wanajeshi rehani," taarifa ya jeshi imesisitiza.

Mhariri Mkuu wa Daily Trust, Mannir Dan-Ali amesema uvamizi wa ofisi za gazeti hilo katika miji ya Maiduguri na mji mkuu wa Abuja umefanyika "kinyume cha sheria".

Wanajeshi walitimua wafanyakazi kutoka ndani ya ofisi hizo na kupora kompyuta kadhaa ambazo waliondoka nazo, alisema Ali katika taarifa yake.

 

 

Advertisement