Kagame aziwakia taasisi za haki za binadamu

Rais wa Rwanda, Paul Kagame amezipuuza shutuma za taasisi za haki za binadamu katika nchi za magharibi dhidi ya nchi yake akisema ni takataka na kichekesho.

Akizungumza katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha France24 cha Ufaransa, Kagame Rwanda ni tofauti sana na ilivyokuwa miaka 25 iliyopita lakini taasisi hizo hazioni.

Aliwataka waendeshaji wa kipindi hicho kuangalia kile alichosema ni rekodi iliyoshindwa ya haki za binadamu Ulaya, hasa katika kushughulikia wahamiaji.

“Ulaya inakiuka haki za binadamu, kwa hii tabia ya watu kupakiwa kurejeshwa na kuachwa wazame katika Bahari ya meditterrania na wengine wengi wananyanyaswa katika nchi yako,” alisema.

Kagame alisema shutuma za Ulaya zinatokana na hisia kuwa wenyewe wako safi kuliko uhalisia. Hakika mnahitaji kuachana na ujinga wa hizo hisia kuhusu haki za binadamu.

“Mnadhani ni nyinyi pekee mnaoheshimu haki za binadamu, wengine wote wanazikiuka. Hapana, tumepigania haki za binadamu na uhuru kwa ajili ya watu wetu vizuri zaidi yenu ninyi mnaokaa kusema huu upuuzi,” alisema.