Kanisa Katoliki kujadili wanaume waliooa kuwa makasisi Amazon

Tuesday June 18 2019

Vatican. Kanisa Katoliki Duniani linaangalia uwezekano wa kuwafanya wanaume wazee waliooa kuwa makasisi katika maeneo yanayozunguka mto Amazon, barani Amerika Kusini.

Hatua ya kanisa hilo inafuatia eneo hilo lenye wakazi karibu milioni 33 kupatikana katikati ya msitu mnene kuwa na uhaba mkubwa wa makasisi licha ya kuwa na wafuasi wengi wa kanisa hilo.

Inaelezwa kuwa iwapo suala hilo litapitishwa, itakuwa ni mabadiliko makubwa ndani ya kanisa hilo kwa kipindi cha miaka 1000.

Mabadiliko hayo yamependekezwa kwenye Waraka muhimu wa Mazingira wa Papa - Laudato Si - uliochapishwa mwaka 2015.

Katika waraka huo, Papa Francis, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki ameandika kuwa, eneo hilo la Amazon linakabiliana na changamoto ambazo (kuzitatua) "inahitaji mabadiliko ya kimfumo na kibinafsi kwa watu wote, mataifa yote (ya eneo hilo la Amazon) pamoja na Kanisa."

Waraka huo unatarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano maalumu wa majimbo ya kanisa hilo kwenye eneo lote la msitu wa Amazon mwezi Oktoba jijini Roma, Italia.

Advertisement

Mkutano huo pia utahudhuriwa na maaskofu na wawakilishi wa waumini wa eneo hilo ambalo linapatikana katika nchi za Brazil, Bolivia, Peru, Ecuador, Colombia, Venezuela, Guyana, Suriname na French Guyana.

Awali kanisa hilo limesema eneo hilo linaibua changamoto kubwa ya kikasisi na kimazingira lakini ni uhaba wa makasisi ambao kanisa linaweza kupata ufumbuzi wake wa moja kwa moja.

Advertisement