Kikosi maalumu kilichozima shambulizi la ugaidi Kenya

Muktasari:

Kikosi hicho cha Recce kilianzishwa mwaka 1965 kwa ajili ya kukabiliana na matukio kigaidi

Nairobi,Kenya. Vikosi maalum nchini Kenya vilivyopata mafunzo ya kutosha vilidhihirika juzi baada ya kuzima shambulizi kwa kusimama imara na kulinda uhuru wa nchi yao.

Vikosi hivyo maalum vya Kenya ambavyo ni pamoja na Recce, RDU, Flying Squad na kile cha KDF vilidhihirisha uwezo mkubwa kukabiliana na hatari yoyote.

Wakenya wameibuka mashujaa na imara zaidi kama taifa, kufuatia shambulizi la kigaidi la Jumanne katika majengo ya hoteli ya Dusit D2 jijini Nairobi kwa kuua magaidi waliokuwa na lengo la kumwaga damu , uharibifu wa mali na taharuki.

Magaidi hao wanaokisiwa kuwa sita waliuawa kwenye operesheni ambayo imepokea sifa kimataifa kutokana na ushujaa wa maofisa wa usalama na raia waliohusika katika shughuli za uokoaji na kukabiliana na wavamizi hao.

Wapiganaji hao wa Kenya walifika kwa haraka katika eneo la tukio na mara moja wakaanza juhudi za kuokoa raia waliokuwa wamekwama katika hoteli hiyo na majengo yaliyo karibu, huku wakikabiliana vikali na kundi hilo ambalo tayari lilishaanza kuua na kujeruhi wengine.

Hali ingekuwa mbaya zaidi kama si juhudi za vikosi hivyo kufika hapo kwa haraka, pamoja na kutekeleza shughuli hiyo kwa utaalamu mkubwa bila uwoga.

Vikosi hivyo vilifanikiwa kuokoa watu zaidi ya 700 na mpaka juzi asubuhi walikuwa wamewaua wavamizi wote.

Wakati vikosi hivyo vikiendelea na kazi pia polisi wa kawaida, GSU na AP pia walitekeleza wajibu wao muhimu katika operesheni hiyo ya kipekee kwa kuweka ulinzi mkali nje ya majengo hayo, kudhibiti raia, kusaidia katika kufanikisha manusura kupelekwa hospitalini na kuwahoji waliookolewa.

Mbali na kuwasili eneo la shambulizi kwa haraka, askari wa vikosi hivyo vya usalama walielewana vyema tofauti na walivyoshughulikia shambulizi la Westgate ambapo watu 67 waliuawa na la Chuo Kikuu cha Garissa ambapo watu 147 walipoteza uhai.

Mbali ya askari hao lakini pia askari wa uokoaji wakiongozwa na Shirika la Msalaba Mwekundu na madereva wa magari ya wagonjwa nao walichangia kiasi kikubwa katika shughuli hiyo kwa juhudi zao za kuwapatia majeruhi huduma ya kwanza na kuhakikisha wamepelekwa hospitalini.

Juhudi hizo zilisaidia kuokoa maisha na kupunguza mishtuko miongoni mwa waliookolewa.

Pendekezo la kuunda kikosi maalumu cha Recce katika kitengo cha GSU lilianza kutolewa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bruce Mckenzie mwaka 1964 wakati wa Utawala wa Jomo Kenyatta.

Kikosi cha kwanza cha askari 37 wa Recce wa kumlinda Jomo Kenyatta kiliundwa 1965. Maofisa hao wote walikuwa wakitoka jamii ya Wakikuyu.

Mnamo mwaka 1966, Serikali ya Uingereza ilimtaka Kenyatta kuongeza maofisa 20 wa Recce kutoka jamii nyinginezo ilmradi wawe waaminifu kwake.

Na sasa, sasa kikosi cha Recce kimeweka kambi katika eneo la Ruiru na kwa kawaida hutumia bunduki aina ya M16 ambazo hutengenezewa Marekani.

Kwa kawaida kikosi hiki maalumu hutumwa kusaidia vikosi vingine vya polisi wa GSU. Na Hutekeleza majukumu yanayohitaji uangalifu mkubwa kama vile uokoaji wa watu waliotekwa na magaidi.

Awali walitumika baada ya uvamizi wa Jumba la Maduka la Westgate (2013), Chuo Kikuu cha Garissa (2015) na shambulio la Jumatatu katika Hoteli ya Dusit D2, Nairobi.

Mafunzo wanayopata

Hupewa mafunzo ya hali ya juu na kikosi hicho kinakadiriwa kuwa na askari 500. Askari huanza kwa kupewa mafunzo ya kawaida katika Chuo cha Mafunzo cha Embakasi.

Miongoni mwa mambo wanayofundishwa ni kutegua mabomu, usalama wa ndani ya majengo, kukabiliana na magaidi, kukabiliana na watekaji nyara wa ndege na uokoaji.

Recce hupata mafunzo ya ziada Israeli, Marekani, chuoni Ruiru, katika eneo la Solio Ranch na kambi ya mafunzo ya magadi.

Baada ya mafunzo, askari hao hugawanywa makundi matatu kulingana na eneo walilofuzu. Kikosi cha kwanza ni kile cha kukabiliana na watekaji nyara wa ndege na ugaidi. Kikosi kingine ni kile cha kukabiliana na mikasa huwa tayari kusaidia polisi wa kawaida wanapoelemewa.

Kikosi cha mwisho ni kile cha kulinda watu mashuhuri na hupata mafunzo nchini Israeli na Marekani. Kikosi hiki ndicho kilihusika kutoa ulinzi kwa kiongozi wa Marekani Barack Obama alipotembelea Kenya 2015.

Askari wa Recce huvalia vikoti vyenye mifuko ya kubebea magazini za risasi na huunganishwa na jaketi la kuzuia risasi kupenya.

Al shabaab

Kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na Al Qaeda limesema shambulizi hilo ni jawabu kwa hatua ya Rais Donald Trump.

Kundi hilo kwenye ujumbe wake lilisema Marekani inatakiwa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo ilisema maslahi ya kiuchumi ya Marekani na Israel yataendelea kupata pigo endapo nchi hizo zitaendelea kuzihujumu haki za Wapalestina.

Mara tu baada ya tukio hilo huku jitihada za kuoa wananchi waliokwama kwenye jengo hilo zikiendelea, msemaji wa Al-Shabaab alipiga simu kwenye Kituo cha Habari cha BBC na kudai kwamba kundi hilo limehusika na uvamizi huo.