Kumekucha Marekani, Democratic waanza mbio za kumng’oa Rais Trump

Tuesday June 18 2019

 

Washington, Marekani. Chama cha Democratic cha nchini Marekani kimeanza mchakato wa kutafuta mgombea wa nafasi ya uras.

Chama hicho kimeanza kampeni zake wakati miaka minne ya Rais Donald Trump inaelekea ukingoni na mwakani, 2020, ni Uchaguzi Mkuu mwingine huku ikitarajiwa kuwa Rais Trump atawania muhula wa pili wa miaka minne kupitia.

Alhamisi iliyopita chama hicho kilipuliza kipenga cha kuanza mchakato wa kutafuta mgombea urais.

Kamati Kuu ya Democratic ilipitisha majina ya watu 20 kushiriki midahalo miwili ya hatua za awali za kusaka mgombea.

Democratic ilipoteza kiti baada ya Barack Obama kumaliza muda wake na mgombea aliyemfuatia, Hillary Clinton kupoteza dhidi ya Donald Trump.

Midahalo hiyo inayosubiriwa kwa hamu na Wamarekani inatarajiwa kufanyika Miami usiku wa Jumatano na Alhamisi (Juni 26 na 27).

Advertisement

Kamati hiyo iliweka utaratibu wa kupata mshindi tangu Januari mwaka huu, ukimtaka kila mgombea kuwa na wadhamini 65,000 na walau asimilia moja ya kura za maoni.

“Tuliweka utaratibu mapema. Tulieleza taratibu hizo kwa wazi na kwa kila mtu. Hatukupata ukinzani wowote tulipozieleza,” alisema Mwenyekiti wa Democratic, Tom Perez akifafanua madai kuwa kuna taratibu zimekiukwa.

Katika orodha yake, chama hicho kimepanga waombaji 10 kila mdahalo, wakiwamo wanawake watatu katika siku ya kwanza na wengine watatu siku ya pili.

Watakaochuana katika mdahalo siku ya kwanza ni Cory Booker, seneta New Jersey; Julián Castro waziri wa zamani wa nyumba;  Bill de Blasio, meya wa Jiji la New York; John Delaney, mwakilishi wa zamani wa Maryland na mwakilishi wa Hawaii, Tulsi Gabbard.

Wengine ni Gavana wa Washington, Jay Inslee; Seneta Minnesota, Amy Klobuchar; mwakilishi wa zamani wa Texas, Beto O’Rourke; Mwakilishi wa Ohio, Tim Ryan na seneta Massachusetts, Elizabeth Warren.

Katika mchuano wa pili, pamoja na watu wengine, atakuwamo makamu wa rais wa zamani (kwa Bill Clinton), Joe Biden; na wengine tisa ambao ni Michael Bennet, seneta wa Colorado; Pete Buttigieg, meya wa South Bend, Ind., Kirsten Gillibrand, seneta New York; Kamala Harris, seneta California na gavana wa zamani wa Colorado, John Hickenlooper.

Advertisement