Mafuriko yaua 17 Uganda

Muktasari:

  • Wengi wamesombwa na maji ya mto, huku nyumba zao zikianguka

Buyende, Uganda. Watu 17 wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali ya upepo wilayani  Buyende nchini Uganda, huku wengi wa waliofariki wakitokea  kijiji cha Kidera.

Mwenyekiti wa Kaunti ya Kidera, William Kiiza amesema  huenda idadi ya  watu waliopoteza maisha ikaongezeka.

“Niliyoihesabu mimi ilikuwa 17 na wengine ambao wamepelekwa hospitalini ni zaidi ya 80, lakini huenda idadi hiyo ikaongezeka,” amesema.

Kiiza amesema kikosi cha uokoaji kinaendelea kazi huku waliopata majeraha wakipelekwa Kituo cha Afya Kidera na Hospitali ya Kamuli.

Mvua hiyo imevunja nyumba za watu na kusababisha wengi kukosa makazi.

Eneo la Tororo, wakazi wa kijiji cha Amoni mjini Malaba walikuta miili ya watu ikisombwa na maji kuelekea mto Malaba.

Mashuhuda wameliambia gazeti la Daily Monitor kuwa kuna raia mmoja alisomwa na maji wakati akichuma mboga mtoni hapo.

 Selestino Obbo, ni miongoni mwa watu walionusurika amesema watu wengi waliokuwa wakichuma mboga kwenye bustani walisombwa na maji, lakini yeye alifanikiwa kupanda mti uliokuwa karibu na mto huo.

Mzazi wa watoto wawili ambao wamesombwa na maji hayo, Milton Epiu alisema watoto wake walikufa wakati yeye akiwa baa.