Majanga 9 yalivyoitikisa Dunia

Tuesday March 19 2019

 

Mashirika. Mashirika. Dunia imeonekana kuhemewa na matukio ya aina mbalimbali, ikiwamo yale yaliyoshtukiza na kuleta simanzi huku mengine yakiendelea kuacha maswali vichwani mwa wengi.

Matukio hayo ambayo mengine yakisababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali na mazingira, yanatajwa kama moja ya mambo yaliyotikisa katika kipindi cha Februari mpaka Machi.

Katika kipindi cha wiki mbili matukio ya ukame, mauaji ya watu wengi, utekaji watoto, ajali ya ndege na njaa ni mambo yaliyochukua sehemu kubwa katika taarifa za vyombo vya habari kutokana na namna yalivyoibuka katika sehemu mbalimbali duniani.

Nchi ambazo zimekumbwa na majanga hayo hivi karibuni ni pamoja na Kenya, Ethiopia, New Zealand, Zimbabwe, Msumbiji na Malawi.

Utekaji watoto Tanzania

Mauaji ya watoto yalitikisa mikoa ya Njombe na Simiyu kwani watoto walikuwa wakitekwa na watu wasiojulikana na kuzua hofu kwa familia zinazoishi Tanzania hususan mikoa hiyo.

Mratibu wa Jukwaa la Mashirika ya Kutetea Haki za Watoto Erick Giga alisema kwamba “Kuna changamoto za uelewa ambapo elimu inatakiwa kutolewa kwa watoto shuleni na majumbani kuhusu hali hatarishi na namna gani ya kujikinga nazo.

Njaa inavyotikisa Kenya

Zaidi ya watu 10 wameripotiwa kufariki kutokana na ukame katika kaunti ya Turkana nchini Kenya, wengine zaidi ya 800,000 wakiendelea kuumia kwa makali ya njaa na kiu kwa mujibu wa wizara ya kudhibiti majanga na utumishi wa umma ya kaunti ya Turkana.

Serikali ya kaunti hiyo wiki iliyopita ilitoa hakikisho kwamba imeidhinisha mpango wa usaidizi kuwakinga wakaazi kutokana na madhara ya ukame uliopo.

India yaishambulia Pakistan

Ndege za India zilishambulia kwa mabomu kambi za wanamgambo zilizoko katika ardhi ya Pakistan ya eneo linalogombewa la Kashmir na kuongeza makali katika mvutano mkubwa wa kidiplomasia baina ya nchi hizo

Ajali ya ndege Ethiopia

Ibada zimefanyika katika mataifa ya Ethiopia na Kenya kwa ajili ya kuwaombea watu 157 waliopoteza maisha kwenye ajali ya ndege ya Ethiopia Airlines iliyoanguka Machi 10.

Wafanyakazi wa Ethiopian Airlines walikusanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Bole International kutoa heshima zao za mwisho za wahudumu wa ndege ya Boeing 737 MAX 8 chapa 302 iliyokuwa ikieelekea katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

New Zealand

Raia mmoja wa Australia aliyefahamika kwa jina la Brenton Tarrant (28) akiwa na wenzake wamevamia misikiti miwili iliyopo nchini New Zealand na kuua watu 49 na kujeruhi wengine 38.

Kijana huyo alikuwa anaonyesha mauaji hayo mubashara katika mtandao wa kijamii wa Facebook kupitia kamera aliyokuwa ameivaa kichwani.

Mshambuliaji huyo alionyesha shambulizi hilo baada ya kuchapisha msimamo wake ambapo amewaita wahamiaji ni wavamizi. Mitandao ya jamii iliamrishwa mara moja kuondoa picha hizo za mauaji ya kinyama.

Kimbunga Idai

Idadi kubwa ya watu 100 wamepoteza maisha kutokana na kimbunga Idai nchini Msumbiji na Zimbabwe, Malawi na maofisa katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika wamesema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka, kwa sababu bado watu wengi hawajulikani walipo.

Vifo 62 vimeripotiwa nchini Msumbiji na vingine 65 nchini Zimbabwe, baada ya kimbunga hicho cha kitropiki kupita katika nchi hizo Ijumaa na Jumamosi wiki iliyopita.

Kilitua kwanza katika mkoa wa kati wa Msumbiji usiku wa Alhamis kabla ya kuenea hadi Zimbabwe. Waziri wa Mazingira wa Msumbiji Celso Correia ameliambia shirika la habari la AFP kwamba vifo hivyo vilitokea katika mji wa pwani wa Beira, na katika wilaya ya Dondo ambayo iko bara.

Mauaji DRC

Watu 11 waliuawa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mapigano yaliyotokea kati ya wanajeshi na wapiganaji wa kundi lenye silaha ambalo halijulikani.

Msemaji wa jeshi katika jimbo la Ituri, Jules Ngongo, alisema watu wengine sita walijeruhiwa wakati mapigano hayo yalipozuka kwenye mji wa Torgess katika jimbo hilo.

Uji waua Uganda

Wananchi kadhaa wa Uganda wanaoishi maeneo ya Karamoja wamepoteza maisha baada ya kunywa uji ikiwa ni chakula cha msaada kilichotolewa na Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa (WFP)

Advertisement