Jina la Rais, Odinga, Matiang’i yatajwa sakata la dhahabu feki

Nairobi. Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), Noordin Haji ameonya kuhusu sauti ya mawasiliano inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikitaja jina la Rais kuhusika na sakata la dhahabu feki aliyotapeliwa Mwanamfalme wa miliki ya Kiarabu (UAE), Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum.

Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo, DPP amewaonya wananchi waache kusambaza kwenye mitandao ya kijamii rekodi ya mawasiliano kati ya watu wawili kuhusiana na sakata hilo.

Sakata hilo linalohusisha raia wa Kenya, Tanzania, Nigeria na Congo hivi sasa linachunguzwa na polisi wa Kenya na DPP amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Hilary Mutyambai kukamilisha uchunguzi ndani ya siku saba.

“Hisia zangu zimevutiwa na kanda ya sauti inayozungushwa mitandaoni ambapo madai yanayotolewa na watu wawili wanaozungumza kuashiria kuwa habari fulani ziliwasilishwa kwa Rais, aliyekuwa waziri mkuu na waziri Matiang’i.”

“Madai kama hayo, na kusambazwa kwayo kupitia mitandao ya kijamii, hayafai kwa sababu yanaweza kuzua taharuki bila sababu yoyote,” alisema DPP.

DPP alisema ni makosa kusambaza rekodi za mawasiliano kama hizo kwa umma hadi pale ukweli wote utakapo patikana na kuchambuliwa.

Alisema amepokea malalamiko kutoka kwa waathirika wa tukio hilo wakidai kuwa watu waliotajwa wamekuwa wakiwasiliana nao kwa muda sasa huku wakitaja jina la Rais katika shughuli zao na mawasiliano.

“Baada ya kugundua kuwa walihadaiwa kuhusu uwepo wa dhahabu na madai ya uwongo kwamba Rais, aliyekuwa waziri mkuu na Waziri Fred Matiang’i walifahamu kuhusu shughuli hizo, waliamua kutoa ripoti kwa maofisa wa Kenya. Pia, waliamua kushirikiana na walinda usalama kufichua ukweli kuhusu shughuli hizo,” akasema Haji.

DPP alitoa wito kwa Wakenya ambao wanaweza kuwa na habari kuhusu sakata hizo kutoa ripoti wa asasi za usalama, ili kulinda hadhi ya uchunguzi unaoendelea sawa na ushahidi na mashahidi.

“Lengo la uchunguzi wowote wa kitendo cha uhalifu ni kuhakikisha washukiwa wanawajibika. Hii inaweza tu kufanyika wakati ambapo uchunguzi unaendeshwa katika mazingira tulivu, pasina uvumi na vitisho. Kwa sababu hiyo, naomba kila mmoja aliye na habari ambazo zinaweza kusaidia katika uchunguzi unaoendelea kuziwasilisha kwa asasi zinazoendesha uchunguzi,” DPP.

Pia, aliahidi kuchukua hatua za kisheria kwa washukiwa pindi atakapopokea faili hiyo. Mmoja wa washukiwa hao ni Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula.