Malaysia kutengeneza magari yanayopaa

Wednesday February 27 2019

 

Kuala Lumpur, Malaysia. Malaysia inapanga kuzindua magari yanayopaa, waziri amesema leo na kusababisha kuibuka kwa kejeli katika nchi hiyo ambayo ina historia tofauti katika masuala ya miradi ya magari.
Mfano wa gari hilo, ambalo linatumia teknolojia ya nchini Malysia, unatarajiwa kuwekwa bayana mwishoni mwa mwaka, alisema Waziri wa Maendeleo ya Biashara, Redzuan Mohamad Yusof alipoongea na Shirika la Habari la Serikali la Bernama.
Kutengeneza gari hilo kunagharimu dola 245,000 (sawa na zidi ya Sh500 milioni za Kitanzania) na itakuwa haipai juu sana, alisema bila ya kutoa taarifa zaidi.
Mipango iliyopita nchini Malaysia haikuwa na mafanikio makubwa, ilianza kutengeneza magari aina ya Proton miaka ya 1980 lakini yanakosolewa kwa kuwa na umbile baya na umaarufu wake umeshuka kwa kasi.
Kwa wengi, mpango wa magari hayo ni mradi mwingine ambao haukufikiriwa vizuri na umetengenezwa na wanasiasa wajinga.
"Sina maneno. Sijawahi kusoma maneno ya kijinga mengi maishani mwangu," alisema mmoja wa wakosoaji.
Aman Shah, aliandika katika ukurasa wa Facebook akisema: "Inawezekanaje mpumbavu huyo akateuliwa kuwa waziri? tatua tatizo la usafiri wa umma kwanza badala ya kubuni magari yanayopaa."
Kumekuwa na majaribio kadhaa duniani ya kutengeneza magari yanayopaa, kama lile la Transition lililotengenezwa na kampuni ya Marekani ya Terrafugia na gari aina ya AeroMobil, lililotengenezwa nchini Slovakia.
Yote yamechukua miaka kadhaa na kutumia fedha nyingi kuyatengeneza na bado hayajaingia sokoni.
Baadhi walihoji busara ya kujaribu kutengeneza gari linalopaa nchini Malaysia wakati sekta ya magari katika taifa hilo ikiwa tayari inakumbana na matatizo.
"Hatuwezi hata tukatangaza magari tunayotengeneza ya umeme na kuyauza kwa bei nafuu, halafu tunazungumzia magari yanayopaa. Kituko gani hiki," alisema mmoja wa wakosoaji.
Tangu arejee madarakani kwa kipindi cha pili, Waziri Mkuu, Mahathir Mohamad ambaye awali aliongoza mpango wa kutengeneza Proton, ameeleza mpango mpya wa taifa wa kuendeleza sekta ya uzalishaji magari.

Caption
Wapenzi wakipiga picha wakiwa katika chumba cha vioo katika moja ya majengo marefu jijini Kuala Lumpur siku ya wapendanao. AFP

Advertisement