Mama amsahau mtoto airport, ndege yageuza angani kumfuata

Muktasari:

  • Rubani amelazimika kuwaomba abiria kumrudia mtoto huyo ambaye alisahauliwa na mama yake uwanja wa ndege wa Saudi Arabia

Saudi Arabia. Si jambo la kushangaza sana kusahau begi, simu au pochi katika uwanja wa ndege. Hakuna atakayekulaumu kwa kusahau vitu hivyo.

Katika hali isiyo ya kawaida rubani wa ndege amelazimika kuirudisha ndege uwanja wa ndege baada ya abiria mmoja kumsahau mtoto wake uwanja wa ndege wa kimataifa wa King Abdulaziz uliopo Jeddah nchini Saudi Arabia.

Taarifa zilisema kwamba ndege hiyo ya Saudia SV832 ilirudi baada ya abiria huyo kuwaambia wahudumu wa ndege kuwa amesahau mtoto wake sehemu ya mapumziko ya uwanja wa ndege na kwamba hayupo tayari kuendelea na safari hiyo.

Ndege hiyo iliyokuwa imetoka Jeddah kwenda Kuala Lumpur ilibidi igeuze ikiwa tayari angani baada ya mazungumzo ya rubani na maofisa wa kuongoza ndege waliokuwa uwanja wa ndege wa Jeddah.

“Mola awe nasi, tunaomba kurejea uwanja wa ndege,” inasikika sauti ya rubani ikiomba kurejea na kuwaacha maofisa wa kuongoza ndege waliokuwa uwanjani wakishangaa na kushauriana.

Mmoja wa waongoza ndege anasikika akiomba ushauri kwa wenzake huku akisema, “kuna abiria kasahau mtoto wake hapa, maskini!”

Rubani anasikika akisisitiza tena, “nimekwambia kuna abiria kasahau mtoto wake hapo uwanjani na hataki kuendelea na safari, nataka kurudisha ndege.”

Baada ya mazungumzo mafupi, rubani huyo aliruhusiwa kurudi katika uwanja wa ndege ambako inasemekana abiria huyo aliungana na mwanaye.

Tukio la kushangaza kama hilo lilitokea mwaka 2013, wakati ndege ya Marekani ‘American Airlines’ iliyokuwa ikitoka Los Angeles kwenda New York ilipolazimika kutua katika uwanja wa mji wa Kansas kutokana na abiria mmoja kugoma kuacha kuimba wimbo wa I will Always Love You wa Whitney Houston.