Marekani yatishia kuwafunga majaji wa ICC

Tuesday September 11 2018

 

Washington, Marekani. Marekani imetishia kuwakamata na kuwawekea vikwazo majaji na maofisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ikiwa wataendelea kufanya uchunguzi juu ya uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na askari wa Marekani nchini Afghanistan.


Kauli hiyo ilitolewa Jumatatu na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa katika Ikulu ya White House, John Bolton alipowahutubia wanachama wa kundi la kihafidhina la Federalist Society jijini Washington.
"Leo (Jumatatu), siku ya mkesha wa Septemba 11, nataka kutoa ujumbe uliowazi na usio na utata kwa niaba ya rais. Marekani itatumia njia zozote kuwalinda raia wake na wa washirika wake dhidi ya mashtaka yasiyo ya haki yanayoandaliwa na Mahakama batili,” alisema Bolton.
"Hatutashirikiana na ICC. Hatutatoa usaidizi wowote kwa ICC ...Tutaiacha ICC ijifie yenyewe. Isitoshe, kwa dhamira na malengo yawayo yote, kwetu sisi ICC imeshakufa."

Uhalifu Afghanistan
Mwaka 2016, mahakama hiyo ya The Hague ilisema upo uwezekano baadhi ya askari katika vikosi vya Marekani na shirika la CIA walitenda uhalifu kwa kuwatesa watu waliokuwa wanashikiliwa Afghanistan.
Ikiwa imeanzishwa mwaka 2002 chini ya Mkataba wa Rome, ICC ndiyo mahakama ya kwanza duniani iliyoundwa kwa ajili ya kuendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari.
Zaidi ya nchi 120 duniani ni wanachama wa ICC lakini mataifa yenye nguvu - Marekani, China na Urusi – zilikataa kutia saini.
Bolton alisema ikiwa uchunguzi utaendelea dhidi ya Marekani juu ya uhalifu wa kivita, utawala wa Trump utafikiria kuwazuia majaji na waendesha mashtaka kuingia nchini, kuwawekea vikwazo vya fedha wanazopata kupitia mfumo wa Marekani na kuwashtaki katika mahakama za Marekani.

Advertisement