Marekani yaja juu kuhusu Bobi Wine, Uganda yajibu

Muktasari:

  • Serikali ya Uganda imesema kwamba hakuna wa kuwafundisha kuhusu haki za binadamu na imeitaka Marekani kuangalia historia yake ya uvunjifu wa haki za binadamu

Kampala,Uganda.Marekani imeshutumu unyanyasaji wa wanasiasa wa upinzani  unaofanywa na Serikali ya Uganda, ikisema kwamba ni kinyume cha Katiba ya taifa hilo.

Taarifa iliyochapishwa katika website ya ubalozi wa Marekani inaituhumu Serikali ya Uganda kuwakamata watu pasipo sababu na kuitaka kuheshimu uhuru wa kujieleza kama katiba inavyoruhusu.

Hatua hiyo ya Ubalozi kutoa tamko hilo ni baada ya polisi kumzingira Mbunge wa Kyadondo Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine huku ikitaja pia tukio la kuzuiwa nyumbani kwake kiongozi wa upinzani nchini humo, Dk Kiiza Besigye.

“leo tunaungana na raia wa Uganda kuihoji Serikali ya Uganda kwanini walimzuia Bobi Wine kufanya onyesho lake siku ya Pasaka? Huu ni uonevu na uvunjifu wa amani na pia ni ukiukwaji mkubwa wa katiba ya nchi,’’ imesema sehemu ya ujumbe huo.

Ujumbe huo umesema kwamba maandamano ambayo Bobi Wine alitangaza kuyafanya yalikuwa ya amani lakini ikatumika nguvu kubwa ya dola kuyazuia bila hata kujali amani kwa raia.

 

Polisi kwa watati tofauti walimzuia Dk Besigye kuhojiwa na radio na pia kumzuia Bobi Wine kufanya onyesho lake mjini Kampala na maeneo mengine.

Sasa hivi Bobi Wine yuko kwenye kifungo maalum nyumbani kwake Magere, wilaya ya Wakiso ambapo imezungukwa na askari, huku polisi wakisema kwamba ni amri kutoka juu.

Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kasangati,  Raphael Magyezi amesema kwamba ni amri kutoka juu kuhakikisha kwamba mwanasiasa huyo hatoki nyumbani kwake.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje, Okello Oryem amesema kwamba ubalozi wa Marekani hauna mamlaka ya kuifundisha Uganda kuhusu haki za binadamu.

“Hakuna anayeweza kutufundisha sisi (Uganda) kuhusu haki za binadamu  wao wenyewe (wamerekani) wajiangalie wenyewe rekodi zao za uvunjifu wa haki za binadamu,’’ amesema.