Mbunge ataka wabakaji wakatwe nyeti

Saturday April 13 2019

 

Lamu, Kenya. Mbunge mwakilishi wa Wanawake wa Lamu katika Bunge la Kitaifa, Ruweida Obo amependekeza wanaume watakaopatikana na hatia ya kuwanajisi wasichana wa umri mdogo waadhibiwe kwa kukatwa sehemu zao za siri.

Obo amesema adhabu kama hiyo ndiyo inayostahili kwa watu kama hao ambao wanaamua kufanya makosa kama hayo kwa makusudi.

“Mtuhumiwa  akipatikana na hatia ya kunajisi na kubaka kisha ashtakiwe na kufungwa miaka 20 hukumu hiyo haitoshi ukizingatia madhara wanayopata watoto wadogo wanaobakwa,” amesema.

“Hii ndiyo maana ninapendekeza ukataji wa viungo vyao hivyo vinavyowashawishi wabakaji hao. Na kama mbunge nitawasilisha muswada bungeni kuhakikisha kuwa sheria ya kuidhinisha adhabu hiyo inaanzishwa,” amesema.

Februari Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Isiolo, Rehema Jaldesa alitoa pendekezo kama hilo, akisema hiyo ndiyo njia ya kipekee ya kutokomeza suala la ubakaji hasa miongoni mwa jamii za wafugaji.

Advertisement