Miili ya waliofariki ajali ya ndege yawekwa kwenye mifuko

Muktasari:

Shughuli za kukusanya miili hiyo ambayo ilikuwa ikiwekwa kwenye mifuko maalum bado inaendelea huku wafanyakazi wa Wizara ya Afya ,Msalaba mwekundu na maofisa wengine wa Serikali ya Ethiopia wakiwa eneo la tukio

Addis Ababa,Ethiopia. Shirika la Msalaba Mwekundu  la Ethiopia limefanikiwa kupata miili ya watu waliokuwa kwenye ajali ya ndege ya  Shirika la Ethiopia  iliyotokea leo saa mbili asubuhi  baada ya  ndege hiyo kupoteza mawasiliano  ikiwa angani.

Ndege aina ya Boeing 737-Max 8 iliyopata ajali leo asubuhi ilikuwa ni ndege mpya, iliyokabidhiwa kwa shirika la ndege la Ethiopia Julai mwaka jana.

Wakati ikipata ajali ndege hiyo iliyokuwa na abiria 149 na wafanyakazi wanane. Ilikuwa ikitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole Addis Ababa nchini Ethiopia kwenda uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi nchini Kenya.

Wafanyakazi wa msalama mwekundu wameokena wakifanya kazi bila kupumzika kuhakikisha wanakusanya miili hiyo ya watu waliopoteza maisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la ndege la Ethiopia, ndege hiyo iliruka saa 2:38 asubuhi kwa saa za Ethiopia kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole na kwamba watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wanatoka katika nchi 33.

“Kwa wakati huu, operesheni ya utafutaji na uokoaji miili zinaendelea na hatuna taarifa zilizothibitishwa za waliopona au waliojeruhiwa kwenye ajali hii. Wafanyakazi wa shirika hili wamekwenda eneo la tukio na watafanya kila linalowezekana kutoa huduma za dharula,” inasomeka sehemu ya taarifa ya shirika hilo.

Msemaji wa Shirika la Ndege  Asrat Begashaw alinukuliwa na Shirika la Habari la Kitaifa la Ethiopia akithibitisha kwamba hakuna abiria hata mmoja aliyenusurika katika ajali hiyo, wote wamekufa.