Mkenya matatani kwa kuwaua wanawake 11 Marekani

Monday May 20 2019

 

Nairobi. Raia wa Kenya anayeishi nchini Marekani amefunguliwa mashtaka ya kuwaua wanawake 11 wakongwe na kuiba mali ya thamani kubwa, eneo la Dallas, Texas.

Billy Chemirmir mwenye umri wa miaka 46 alikamatwa kufuatia mauaji ya mwanamke wa miaka 81, na amefunguliwa mashtaka sita, kuhusu mauaji ya wanawake wa kati ya miaka 76 na 94.

Kulingana na mashirika ya habari nchini Marekani, Chemirmir amekuwa kizuizini kutoka Machi 2018 kuhusiana na mauaji ya Lu Thi Harris, 81, ambaye alikuwa mkazi wa Dallas.

Polisi wanadaiwa kupata ushahidi uliomhusisha na mauaji ya Harris, wakati alipokuwa akihojiwa kuhusiana na mauaji hayo na mtu asiyeaminika akampigia simu.

Mwanamume huyo aidha anadaiwa kuwa alivunja na kuingia katika nyumba ya ajuza wa miaka 91 Machi 2018 na kusababisha mauaji, ambacho kilikuwa kiini cha kukamatwa kwake.

Mashirika ya habari yaliripoti kuwa mwanamume huyo alimpiga ajuza huyo kwa mto hadi akapoteza fahamu, kisha akaiba mali yake. Wahudumu wa afya walipofika na kumuamsha, ajuza huyo anaripotiwa kuwaambia kuwa mvamizi ndiye aliyepora mali yake.

Advertisement

Polisi walichunguza na kubaini kuwa Chemirmir ndiye alikuwa mvamizi huyo, kisha wakampata na mali hizo, zikiwa ndani ya sanduku linalosemekana lilikuwa limeibiwa kwa Harris.

Inadaiwa kuwa mshukiwa alikuwa akitumia ujuzi wake katika utoaji wa huduma za afya kuwadhulumu wazee, ambao ni viumbe dhaifu katika jamii.

Polisi wanachunguza visa vya mauaji ya maajuza 750, ambavyo havijawahi kutatuliwa, kuona ikiwa kuna uhusiano wowote.

Wakili wake, hata hivyo, alisema kuwa hawajui mahali mashtaka hayo yalitolewa, mbali na lile la Harris ambalo lilifanya akamatwe.

Advertisement