Mkurugenzi Boeing adai wamejifunza ajali ya ndege iliyoanguka Ethiopia

Muktasari:

Amesema wataichukulia ajali hiyo kama somo ili kuboresha usalama wa ndege

Addis Ababa, Ethiopia. Baada ya kutokea ajali ya ndege  ya  Boeing 737 MAX 8 inayomilikiwa na  Shirika la Ethiopia (Ethiopian Airlines) iliyoanguka jana, Mkurugenzi Mkuu mwandamizi wa shirika hilo, Dennis Muilenburg amesema watajifunza kutokana na ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea baada ya ndege hiyo kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa na kuua watu 157 na kwa mujibu wa Muilenburg ajali hiyo itachukuliwa kwa   uzito na kujifunza kutokana nayo ili kuboresha usalama wake.

“Tutajifunza kutokana na ajali hii na kuendelea kuboresha usalama wa ndege zetu. Kila siku mamilioni ya watu hutegemea ndege zetu za kibiashara kusafiri kote ulimwenguni kwa njia salama. Wakati hili halifanyiki sisi huchukulia hali hiyo kwa uzito,” alisema.

Pia alisema, kampuni hiyo imejitolea kutoa usaidizi kwa Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines endapo itahitajika kufanya hivyo.

Pia wakati uchunguzi ukianzishwa kuhusu ajali ya ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Addis Ababa, Ethiopia kuelekea Nairobi, Kenya  Jumapili, maswali yaliibuka upya kuhusu usalama wake.

Mwaka 2018, ndege aina hiyo hiyo ilianguka baharini  Oktoba na kusababisha vifo vya watu wote 189 nchini Indonesia, dakika 13 tu baada ya kuruka angani.

Ingawa kumekuwepo mamia ya ajali za ndege za Boeing tangu miaka ya sabini, ajali hizi mbili zinasababisha wasiwasi kwa kuwa 737 MAX 8 ni kati ya aina mpya zaidi za ndege za Boeing, kwani zilizinduliwa mwaka 2016.