Mnangagwa atuhumu wafuasi wa Grace kutaka kumuua

Wednesday June 27 2018

 

Harare, Zimbabwe. Rais Emmerson Mnangagwa anasema anahisi kundi lenye uhusiano na aliyekuwa mke wa Robert Mugabe, Grace Mugabe kwamba ndilo liko nyuma ya jaribio la kumuua lililoshindwa Jumamosi iliyopita katika mkutano wa hadhara mjini Bulawayo.


Watu wawili walifariki na wengine zaidi ya 40 walijeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu la mkono uliotokea karibu na mahali alipokuwa Mnangagwa muda mfupi baada ya kuhutubia umati wa watu katika eneo linalotajwa kuwa ngome ya upinzani.
Rais Mnangagwa alimwambia mwandishi wa shirika la habari la BBC, Fergal Keane kwamba analituhumu katika jaribio hilo kundi la G40, ambalo lilikuwa likimuunga mkono Grace katika juhudi zake za kutaka kuwa rais.
Mugabe aliondolewa madarakani kwa shinikizo la jeshi Novemba mwaka jana na nafasi yake ilichukuliwa na Mnangagwa. Ulienea uvumi kwamba Grace alikuwa amejipanga kurithi mikoba ya mumewe na kuwa mkuu wa nchi.
Mnangagwa hakumshutumu wala kumhusisha Grace katika jaribio hilo, lakini aliiambia BBC kwamba anatarajia wahusika watakamatwa hivi karibuni.
"Wala sijui kama ni mtu mmoja, nafikiri ni zaidi ya mtu mmoja. Nafikiri ni suala la kisiasa lililopangwa na watu wenye kinyongo,” alisema.
Mnangagwa wakati akiwa makamu wa rais, na Grace walikuwa wanaongoza makundi mawili tofauti ndani ya chama tawala cha Zanu PF ya kuwania mmoja kuteuliwa kuwa mgombea urais kumrithi mkongwe Mugabe. Kundi lililokuwa likimuunga mkono Grace lilijitambulisha kuwa ni Generation 40 kwa kifupi G40 na la Mnangagwa lilijulikana kama Lacoste.
Kundi la G40 lilikuwa likimshambulia Mnangagwa na kuna wakati lilifanya maandamano ya kumpinga na lilichangia kufutwa umakamu wa rais. Pamoja na jaribio hilo Mnangagwa amesema Zimbabwe iko imara.

Advertisement