Msichana wa miaka 18 ajifungua mtoto bila kujua

Muktasari:

  • Hakutarajia kupata mtoto kwa kipindi hiki, alipanga kupata mtoto miaka kumi ijayo

Manchester, Uingereza. Msichana Ebony Stevenson, mwenye umri wa miaka 18, kutoka jiji la Manchester nchini Uingereza amekimbizwa hospitali akiwa mahututi na alipozinduka baada ya siku nne alijikuta amejifungua mtoto wa kike.

Ebony ambaye ni mwanafunzi anayesomea fani ya michezo na mazoezi ‘Sports Physiotherapy’ anasema hakuwahi kujihisi mjamzito katika muda wote alipobeba mimba hiyo na kwamba hajawahi kukosa siku zake za hedhi.

Wataalamu wanaeleza kuwa upo uwezekano wa kisayansi kutokea  kwa hali aliyopitia Ebony ingawa ni kwa wanawake wachache.

Hali ya msichana huyo ilibadilika ghafla Desemba 2, 2018, na kulazimika kukimbizwa hospitali ya Royal Oldham, iliyopo Manchester na ilipofika Desemba 6 alijifungua mtoto wa kike na baada ya tukio hilo alipatwa na mshangao kwani hakujua kwamba ni mjamzito.

“Nilikuwa naona siku zangu kama kawaida, na pia hazijawahi kubadilika, na sikuona dalili yoyote ile ya kwamba mimi ni mjamzito’’alisema Ebony.

Baada ya madaktari kumpima walimgundua kwamba ni mjamzito na wakamwambia mama yake kwamba anatakiwa kujifungua muda mfupi.

Akapelekwa kwenye chumba maalum na ilipofika muda wa kujifungua alibahatika kupata mtoto wa kike muda wa saa saba na nusu.

Alipozinduka aliambiwa kwamba amepata mtoto na alistuka sana lakini alifurahia taarifa hizo na kumpatia mwanae jina la Elodie.