Museveni ampa cheo cha Luteni Jenerali mtoto wake

Muktasari:

  • Museveni tayari ana miaka 74 na ameshakaa madarakani miongo mitatu sasa akiwa mmoja wa viongozi wa Afrika waliokaa madarakani kwa muda mrefu

Kampala, Uganda. Rais wa Uganda Yoweri Museveni amempandisha cheo mtoto wake wa kiume na kufikia cheo cha pili kwa ukubwa zaidi jeshini.

Kainerugaba Muhoozi sasa amepanda kutoka kuwa Meja Jenerali na kufikia Luteni Jenerali katika Jeshi la Uganda.

Kwa cheo hicho sasa Muhoozi mwenye miaka 44 yupo cheo kimoja nyuma ya baba yake ambaye ni Jenerali kamili.

Ndani ya miaka sita iliyopita, Jenerali Muhoozi amepanda vyeo mara tatu. Japo amekuwa mkuu wa vikosi maalumu vya jeshi la Uganda na sasa ni kama mshauri wa Rais wa operesheni maalumu.

Kutokana na kupanda vyeo kwa kasi wanaharakati wanadai ni kielelezo kuwa kuna mpango unaosukwa wa mtoto huyo wa Rais kumrithi baba yake.

Museveni tayari ana miaka 74 na ameshakaa madarakani miongo mitatu sasa, ni mmoja wa viongozi Afrika waliokaa madarakani kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Jenerali Muhoozi amekuwa akikanusha kuwa ana mipango ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa.

Mwaka 2013 kipindi hicho akiwa Brigedia Jenerali na mkuu wa vikosi maalumu Jenerali Muhozi alidai kuwa Uganda haina utawala wa kifalme.

"Uganda hakuna ufalme ambapo uongozi unarithiwa kutoka baba hadi mtoto, uamuzi wa kuamua ambavyo Uganda itaongozwa ni jukumu la wananchi wenyewe si la mtu mmoja kama wanavyosema baadhi ya watu,'' ilisema taarifa yake rasmi.

Mwaka huo, Magazeti ya Daily Monitor na Red Paper yalichapisha barua iliyofichuliwa na ambayo ilikuwa na maudhui ya mpango wa kumrithisha mamlaka mtoto wa Museveni. Barua hiyo iliandikwa na Jenerali mkuu katika jeshi, David Sejusa, akidai kuwa Museveni ambaye amekuwa madarakani  tangu mwaka 1986 anamuandaa mtoto wake kumrithi.

Sejusa, kwa jina jingine Tinyefuza, alikimbilia Uingereza baada ya kudai kuwepo mpango wa kuwaua wanajeshi wanaopinga mpango huo, ingawa madai hayo yalikosolewa na majenerali wengine jeshini.

Magazeti hayo mawili na vituo viwili vya redio vilifungiwa kwa siku 10 kwa kuchapisha barua hiyo.