Mwanaharakati atishia kupinga tena Brexit mahakamani

Muktasari:

Mwaka 2017, Gina Miller alifungua shauri la kuizuia nchi hiyo kuhesabu siku za kuondoka kwenye umoja huo kabla ya kura ya Bunge.

London, Uingereza. Mwanaharakati anayepinga Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (EU) maarufu Brexit aliyeshinda shauri dhidi ya Serikali ya nchi hiyo amesema atarudi tena mahakamani iwapo waziri mkuu ajaye atajaribu kulazimisha kujitoa bila ya makubaliano.

Mwanaharakati huyo ambaye pia ni mfanyabiashara alisema amewaagiza mawakili wake kumtahadharisha mgombea wa nafasi ya waziri mkuu wa nchi hiyo kupitia Chama cha Conservatve, Boris Johnson.

Miller alisema itakuwa ni matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Bunge litazuia sauti za wawakilishi waliochaguliwa na raia.

Hatua ya mwanaharakati huyo inafuatia kauli iliyotolewa na mgombea huyo wakati wa kampeni zake kuwa Uingereza italazimika kuondoka katika umoja huo Oktoba 31 kama ilivyopangwa.

Mwaka 2017 mwanaharakati huyo alifungua shauri la kuizuia nchi hiyo kuhesabu siku za kuondoka kwenye umoja huo kabla ya kura ya Bunge.