Mwili wa baba yake Tshisekedi haujazikwa tangu Februari 2017

Muktasari:

  • Mtoto wake Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi kwa zaidi ya kura milioni saba kati ya kura milioni 18 zilizopigwa ikiwa ni asilimia (38.6%)

Kinshasa, DRC. Ikiwa Rais mteule Felix Tshisekedi ataapishwa kuwa Rais rasmi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) jukumu lake la kwanza atalazmika kuandaa mazishi ya ya kitaifa ya baba yake mzazi aliyepoteza maisha akiwa kwenye matibabu nchini Ubelgiji Februari Mosi, 2017.

Etienne Tshisekedi, aliyekuwa kiongozi wa upinzani DRC alifariki dunia mjini Brussels nchini Ubelgiji akiwa na umri wa miaka 84 akiwa anapatiwa matibabu.

Wiki iliyopita, Tume ya Uchaguzi (Ceni) ilimtangaza mshindi wa urais, mtoto wa Etienne, Felix Tshisekedi.

Etienne alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe waliokuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia ya nchi yake.

Alisimama kidete katika utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Rais Mobutu Sese Seko, ambaye utawala wake ulidumu kwa miongo kadhaa kabla ya kupinduliwa.

Etienne pia alikuwa mpinzani wa Rais Laurent Kabila, ambaye aliingia madarakani mwaka 1997 na mtoto wake, Rais Joseph Kabila, anayemaliza muda wake.

Kutokana na harakati zake za kisiasa za kupambana na udikteta Etienne Tshisekedi alikamatwa mara kwa mara.

Mara tu baada ya Etienne kuzindua chama chake cha UDPC, Rais Mobutu Seseseko alimhamishia kwa nguvu kwenye kijiji kimoja katika jimbo la Kasai mbali na mji mkuu Kinshasa na mtoto wake wakati huo akiwa na miaka 19 alilazimika kukatisha masomo ili kumfuata baba yake.

Akiwa na umri wa miaka 22 Tshisekedi alikimbilia uhamishoni nchini Ubelgiji pamoja na mama yake na ndugu zake. Huku akifanya kazi za vibarua aliendelea na masomo ya biashara na mawasiliano.

Hata alipokuwa nchini Ubelgiji tayari alianza kuwa mwanaharakati wa kisiasa. Na mara kwa mara alikabiliana na wafuasi wa watawala wa nchini Congo.

Kuna taarifa kuwa aliwahi kupambana na polisi wa Ubelgiji waliojaribu kumzuia baba yake kupanda ndege ili kwenda Kinshasa.

Hata hivyo mtoto wa mwanasiasa huyo analaumiwa kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa anakataa kubeba jumuku la kukiongoza chama cha UDPS.kurithi mikoba ya baba yake.