Ndege ya Fly540 yasitisha kupaa baada ya tairi kukwama kwenye shimo

Monday August 12 2019

 

Mombasa. Rubani wa ndege ya Fly540 alilazimika kusitisha zoezi la kupaa kwa ndege hiyo baada ya tairi kunasa katika moja ya shimo lililokuwa katika barabara kuu iliyopo katika uwanja wa ndege wa Manda uliopo Lamu nchini Kenya.

Maofisa wenye vyeo vya chini walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina walisema kuwa wahandisi na wafanyakazi wengine katika ndege hiyo walilazimika kutoa tairi hilo lililonasa kwa kutumia majembe na machepe.

"Ndege ilikuwa karibu kupaa lakini ilikuwa ngumu sana. Rubani alilazimika kuacha zoezi hilo baada ya kugundua kuwa moja ya tairi ya ndege lilikuwa limekwama kwenye shimo kubwa barabarani. Wahandisi na wafanyakazi wa uwanja wa ndege walilazimika kuitwa na kusaidia kusukuma ndege hiyo na kuiweka katika eneo salama ambapo, hatimaye iliweza kupaa,” ofisa mmoja alisema.

Ofisa  wa Fly540 aliyezungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Manda alisema, ukaguzi ulifanywa baadaye ili kuhakikisha kuwa ndege hiyo iko katika hali nzuri baada ya tukio hilo.

"Ndege ilikuwa ikiondoka majira ya saa 12:30 jioni lakini suala hilo lilisababisha kuchelewa kuondoka kwa ndege hiyo badala yake, iliondoka saa 12:54 jioni baada ya ukaguzi kufanywa ili kuhakikisha kuwa tukio hilo halijasababisha suala lingine ambalo lingeweza kuathiri ndege hiyo, "ofisa huyo alisema.

Kufuatia tukio la Jumapili, vyombo vya kusafiri, wadau wa watalii na abiria wameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) kuingilia kati na kuboresha barabara ya uwanja wa ndege wa Manda.

Advertisement

Advertisement