Nguli wa Afro Jazz, Oliver Mtukudzi afariki dunia

Muktasari:

Alilazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja kabla ya umauti kumkuta katika hospitali ya Avenues jijini Harare.

Harare, Zimbabwe. Mwanamuziki nguli na mwanaharakati wa Zimbabwe, Oliver Mtukudzi amefariki dunia leo Jumatano Januari 23, 2019 katika Hospitali ya Avenues mjini Harare.

Mtukudzi aliyejizolea umaarufu duniani kote kwa nyimbo zake kama Neria na Todii  ameacha watoto watano na wajukuu  wawili.

Kampuni iliyokuwa ikisimamia kazi zake za muziki, Gallo Records imesema mwanamuziki huyo aliyetoa albamu 58 enzi za uhai wake, alikuwa akiugua kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mwanamuziki huyo alilazimika kuacha mialiko ya kwenda mataifa mbalimbali duniani kutokana na kuugua kwake.

Muziki wake wa mtindo wa afro-jazz ulivuka mipaka na kupata mashabiki wengi kote duniani.

Alipata umaarufu nchini Zimbabwe kabla ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1980 alipojiunga katika jeshi na mwimbaji mwenza wa Zimbabwe anayeishi Marekani, Thomas Mapfumo.

Mbali na muziki, mwanamuziki huyo maarufu kwa jina jingine la Tuku alijihusisha na harakati za masuala ya haki na utawala bora.